33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KANGI AWA MBOGO AJALI YA KIGWANGALLA

NA waandishi Wetu – mikoani           |            


WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, ametoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua za kisheria madereva wa magari ya viongozi watakaovunja sheria za usalama barabarani kama ilivyo kwa wengine.

Maelekezo hayo aliyatoa jana jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, saa chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kupata ajali iliyomsababishia majeraha na kuchukua uhai wa ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba (32).

Wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea jana alfajiri, ni wasaidizi wa waziri huyo, Michael Lingwa (30) na Ramadhani  Magimba (30).

Ajali hiyo ilitokea wakati dereva akimkwepa twiga aliyeingia ghafla barabarani katika barabara kuu ya Arusha – Dodoma, Kijiji cha Mdori wilayani Babati.

Hii ni ajali ya pili kutokea ndani ya wiki hii, zote zikihusisha magari ya Serikali na kusababisha vifo, majeruhi na kupoteza fedha za walipakodi zilizotumika kuyanunua.

Mapema wiki hii, gari la Serikali lililokuwa likitumiwa na maofisa wa Wizara ya Viwanda na Biashara, lilipata ajali mkoani Geita na kusababisha kifo cha ofisa mawasilino mwandamizi wa wizara hiyo, Shadrack Sagati na wengine kujeruhiwa.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Waziri Lugola alisema taarifa za Jeshi la Polisi zinaonyesha magari ya viongozi wa Serikali yanaongoza kwa mwendo kasi, ikiwamo kuvunja sheria mbalimbali za barabarani.

“Madereva wa magari ya Serikali wanaongoza kwa kutanua barabarani na mwendokasi, Jeshi la Polisi liwachukulie hatua za kisheria madereva hao kama watu wengine,” alisema Lugola.

Kauli ya waziri huyo, iliungwa mkono na Mjumbe wa Baraza la Usalama Barabarani, Hamza Kasongo ambaye alisema; “Dereva akiwa anaendesha STK au STL huwa anajiona ‘special’ (maalumu) sana na kuvunja sheria za barabarani, sasa ndiyo tutaanza nao kwa kuwashughulikia ipasavyo ili kuondokana kabisa na tatizo la ajali nchini.”

KIGWANGALLA  APELEKWA MUHIMBILI

Wakati  Lugola akitoa maelekezo hayo, jana saa 10 jioni  Kigwangalla alisafirishwa kwa ndege maalumu (Air Ambulance) kwenda katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kabla ya kupelekwa MOI, Kigwangalla na wasaidizi wake walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Selian jijini Arusha kwa helkopta, akitokea katika Kituo cha Afya cha Magugu wilayani Babati Vijijini, ambako alifikishwa saa 1:00 asubuhi baada ya kuokolewa kutoka eneo la tukio na askari wa wanyama pori waliokuwa doria.

Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles