Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
MBUNGE wa Ubungo, Saeed Kubenea (Chadema), amesema chama hicho hakitamvumilia kiongozi yeyote anayetaka kurudisha nyuma harakati za kuleta maendeleo na kuwataka wananchi wa jimbo hilo kutoa taarifa za kiongozi anayekwenda kinyume cha taratibu ili aweze kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na wananchi wa Kimara Mavurunza, Kubenea alisema chama hicho kimejipanga kuleta maendeleo katika jimbo hilo, hivyo kuna haja ya kuwa na viongozi waadilifu ili kuweza kufikia malengo.
“Ndani ya jimbo hatutaki watu wanaotukwamisha, hata akiwa chama gani tutamchukulia hatua, hapa Mavurunza kama kuna matatizo na viongozi wenu naomba mtoe taarifa tuitishe kikao ili tuwachukulie hatua zinazostahili,” alisema Kubenea.
Alisema kushirikiana na viongozi wa manispaa wamejipanga kupambana na wizi pamoja na ubadhirifu atakaofanya kiongozi ama mtumishi wa manispaa hiyo.
Alisema wananchi wanapaswa kufuatilia mchanganuo wa fedha, yakiwamo mapato na matumizi kupitia viongozi wao wa serikali za mitaa pamoja na kuwahoji panapokuwa na upungufu ama udanganyifu.
“Sisi tumekuja kuwafanyia kazi, tunataka kuleta maendeleo ambayo hayajaletwa ndani ya miaka hamsini, hatutaki ghiliba, tutapambana na wezi hata kama ni wa chama chetu tutamwajibisha, hatutamvumilia mtu asiye na huruma na wananchi,” alisema Kubenea.
Kwa upande wa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, alisema kitendo cha Manispaa ya Ubungo kujitegemea kitasaidia kuleta maendeleo haraka, kwakuwa fedha zinazopatikana kupitia makusanyo ya kodi zitatumika kutengeneza miundombinu ya eneo hilo tofauti na ilivyokuwa awali.
“Zamani tulikuwa tunakusanya kodi za huku unaandikiwa kikaratasi unaambiwa upeleke fedha ukajenge barabara za Mbezi au Masaki kwa mabwanyenye na kuziacha barabara za huku zikiwa na makorongo, sasa hivi fedha zetu zitatumika kutengeneza miundombinu yetu yenyewe,” alisema Jacob.
Alisema manispaa hiyo yenye kata 14, inakusanya Sh bilioni 106 kwa mwaka ambazo zikitumika vizuri zinatosha kuleta maenedeleo katika eneo hilo.