26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DR CONGO: YAZINDUKA TOKA USINGIZINI HAINA MWELEKEO

Na Shermarx Ngahemera


kinshasaHAKUNA mtu asiyeielewa nchi ya Kongo  na muziki wake ila tu inafahamika  zaidi wakati mwingi kwa mambo mabaya yatokanayo na mwenendo mbaya wa siasa zake.

Wengi wanashangaa utamu wote wa muziki wanaotengeneza wanatunga saa ngapi na kuucheza muziki huo. Kwani ina taswira ya vurugu tupu.

DR Kongo ni kielelezo cha matatizo yanayoyakumba mataifa yaliyo na mali nyingi na hivyo kunyonywa na mataifa makubwa yenye nguvu za kijeshi, uchumi na hila za kisiasa. Nchi hiyo imekuwa matatizoni kabla na baada ya uhuru wake na hivyo watu kusahau lini iliwahi kuwa na amani.

DR Kongo ina kila kitu ila amani kama alivyosema Jane Sibalonza  kwenye wimbo wake wa Dunia, ambao unasema, Ukiwa tajiri utapata kila kitu ila amani.

Ni kweli DR Kongo imekosa amani. Imekuwa ikipigana vita ya watu wengine na si ya kwake. Imelazimika kupigana kulinda mali zake zisiporwe na nchi jirani za Uganda na Rwanda ambazo zina macho kodo kuhusu utajiri wa nchi hiyo.

Habari zote kutoka DR Kongo zina hali moja yaani zimejaa migogoro, mifarakano na vita na hasa eneo la maziwa makuu na la Mashariki. Vita si ngeni lakini vita hiyo iwe na faida kwa nchi si kunufaisha watu wa nje na ajenda zao zisizoisha ili kupotosha ukweli wa mambo.

Wakongo wanaweza kukubaliana kuhusu kila kitu ila kwa mtawala wao. Kwao kila mtu anaweza kuwa kiongozi na hasa urais nafasi ambayo imepiganiwa toka kifo cha Waziri Mkuu wa kwanza Patrice Lumumba mwaka 1961 na imeendelea hivyo hadi leo pamoja na tawala za Josef Mobutu, halafu akaja Mzee Laurent Desire Kabila kabla ya kifo chake na kuingia mwanawe Joseph Kabila, zenye kulenga kupora mali ya Kongo.

Watafiti wa siasa wanasema vifo vyote hivyo ni matokeo ya siasa chafu dhidi ya wananchi wa Kongo.

Mabeberu hawataki kuachia Kongo na hivyo kwa sasa tatizo ni uchaguzi na uvunjaji wa katiba kwa Rais Kabila kutaka muhula wa tatu.

Mambo yalipokuwa magumu aliomba ashughulikie suala la Katiba na huku upinzani ukitaka aiache Serikali barabarani na wenye nguvu waichukue. Kabila amekataa na hivyo kuongeza muda hadi sheria zote muhimu zitungwe ili nchi iachwe kwenye mwafaka. Wa nani?

Rais Joseph Kabila, aliyeko madarakani kuanzia 2001, anazuiwa na vifungu vya ukomo wa madaraka kuendelea na uchaguzi kwani alishashinda mwaka 2006 na 2011.

Anapambana kisiasa na yule aliyekuwa rafiki wa karibu Gavana Moise Katumbi ambaye ameeleza nia yake ya kugombea suala ambalo wafuasi wa Kabila hawalitaki na kumtaka agombee mara ya tatu.

Kwa mbali kitendo cha Jean-Pierre Bemba, mkuu wa mgambo wa Kongo kuonekana ana hatia katika kesi ya uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa makosa kama ya uhalifu kwa binadamu, matumizi ya askari watoto, matumizi ya ngono, ubakaji na unyanyasaji wanawake uliokuwa umezagaa katika eneo la maziwa makuu kwa miaka 20 iliyopita ni changamoto ya kisiasa kwa wengi.

Pamoja na kasheshe za kivita na kuandamwa na magazeti hasa yale ya Magharibi, Kongo imeendelea vizuri kwenye uchumi na iko kwenye vitabu vizuri kwenye taasisi za Bretton Woods za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Mataifa (IMF). Hicho ndicho cha msingi.

Ukiachia mdororo wa mwaka 2009 ambapo uchumi ulikua kwa asilimia 2.8 pekee karibu miaka yote uchumi wake umekua kwa wastani wa si chini ya asilimia 7.7 kwa miaka mitano mfululizo kutokana na taarifa za WB kwani wanasema kelele za mwenye nyumba hazizuii mpangaji  kupata usingizi mnono.

WB imesema hii ni juu ya wastani wa ile ya Afrika Kusini mwa Sahara (SSA) na hivi tunategemea mwaka huu uchumi utakua kwa asilimia 8 na hivyo kufanya Kongo kuwa moja ya nchi zenye kukua kwa haraka zaidi katika dunia hii.

Utajiri uliotamalaki wa madini    

DR Kongo si nchi iliyoendelea zaidi eneo la Maziwa Makuu, lakini rasilimali zake za madini nyingi na zilizotapakaa maeneo mengi ni chanzo kikuu cha uwekezaji na hivyo kuiweka nchi pazuri kiuchumi kwani inayo madini ya vito, dhahabu, almasi, mafuta na madini mkakati.

Nchi ya DR Kongo ni mchimbaji mkubwa wa kobati, koltani, shaba, almasi  na bati  na huuza katika masoko ya dunia.

Wakati watu wengi wanajua uwepo na umuhimu wa madini ya shaba, almasi, bati na dhahabu lakini hawajui mengi kuhusu kobati na koltani ambayo ndio msingi wa mapigano na vita nyingi nchini humo ikigombaniwa nani awe mtawala wa madini hayo na hivyo kuifanya nchi hiyo isiwe imara kisiasa na kutulia hasa Mashariki ya nchi.

 

Vita ya kobati na koltani

Umuhimu wa madini hayo umeyafanya kuwa ni madini mkakati kwa ulimwengu wa sayansi na teknolojia ya kileo kwa kutumika sehemu nyingi nyeti na muhimu.

Kobati hutumika kutengeneza sumaku na  injini za maji, mvuke, hewa na gesi kwa ajili ya ndege au kuzalisha umeme kwani inahimili joto jingi.

Kutokana na takwimu za mwaka 2013 za Savei ya Jiolojia ya US, DR Kongo inazalisha asilimia 48 ya madini hayo duniani na ina hazina ya madini ya kobati asilimia 47 ya dunia.

Koltani ambayo ni kifupi cha columbite tantalum, hutumika katika vitu vinavyobebeka kama simu, viambata kwenye sehemu zilizofanyiwa upasuaji  kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutopata kutu na hivyo hutumika kwenye kompyuta mpakato, vifaa vya kielektroniki   ambazo huwekwa sekwiti ndogo ndogo sana za umeme.

Bei ya juu ya dola 200 kwa kilo imewezesha nchi hiyo kuuza asilimia 17 ya mahitaji ya dunia. Filamu ya ‘Blood Diamonds’ imethibitisha kiwango ni kikubwa zaidi ya hicho kadiri kinavyokwenda sokoni hupoteza uasilia wake na hasa kwa nchi zenye vurugu kama DR Kongo. Mahitaji ya madini hayo ni makubwa kutoka wazalishaji viwandani wa vifaa vya elektroniki.

Kuzingatia hali halisi ya hazina iliyonayo na mahitaji yake, Kongo uchumi wake hautetereki na kuyumba kwani unaweza kuhimili mengi na wakati mwingine hana mshindani.

Uwekezaji wa moja kwa moja toka nje kwenda Kongo ni wastani wa dola bilioni 2.07 kwa mwaka kama Tanzania ingawa mwaka jana ilipungua na kufikia dola bilioni 1.7 kufuatana na Ripoti ya Uwekezaji wa Ulimwengu (WIR) 2016, inayochapishwa na Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

Mwamko

Alama za ushahidi wa kuamka na kuendelea kunathibitishwa na uboreshaji wa miundombinu na ujenzi wa makazi bora katika mji mkuu wa Kinshasa, miji mingine mikubwa inashamiri ustawi kama Lubumbashi, Mbujimai, Katanga  na Kisangani  ambapo majumba marefu na kreni za ujenzi zinashindana na hivyo zinaonesha wazi ustawi wa uchumi.

UN pamoja na kuwa na vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa nchi inajitahidi vile vile kuisaidia kwenye kupata wawekezaji kwa kuwaita kwenye mkutano kwa ajili ya DRC na Maziwa Makuu.

Mkutano uliofanyika Septemba 2013, ulishuhudia zaidi ya nchi 12 zikiwa na nia ya kuona amani ya kudumu ya Kongo iliungana na Afrika Kusini kuunga mkono mkataba uliofanywa na Umoja Mataifa kwa ajili ya usalama na mwenendo wa ushirikiano ukizingatia kuweza kutumia mali asili zilizopo.

Februari mwaka huu wawakilishi kutoka nchi hizo 13, walikutana Kinshasa, makao makuu ya Kongo kujadili masuala ya uwekezaji na miradi  zaidi ya 24, iliainishwa  na kuuzwa kwa wawekezaji wa kimataifa.

Eneo hilo liliuzwa kwa misingi 7 ya ubora wa uwekezaji ikiwamo; uwingi wa mali asili, ardhi ya kilimo, maji tele na mahitaji yanayokua ya chakula, idadi kubwa ya rasilimali ya vijana wenye nguvu na inayokua na daraja la kati lililosoma linalokua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles