28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kofi Annan na hotuba inayowapiga ‘madongo’, Museven, Kagame

kofiMICHAEL MAURUS NA MITANDAO

APRILI 19, mwaka huu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan, alitoa wito kwa viongozi wa mataifa ya Bara la Afrika kujenga utamaduni wa kuachia madaraka pindi muda wao utakapofikia kikomo badala ya kuendelea kung’ang’ania nyadhifa zao kama wanavyofanya baadhi yao.

Kiongozi huyo aliyejizolea sifa kemkem, zaidi ikiwa ni jitihada zake za kutafuta amani katika mataifa mbalimbali duniani, aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Katika hotuba yake hiyo kwa viongozi wa mataifa ya Afrika, Annan alisema kuwa kitendo cha watawala kung’ang’ania madaraka, husaidia kuvipa nguvu vyama vya upinzani ambavyo ni wazi vitakuwa vikipigania kufanyika kwa uchaguzi hali inayoweza kuzaa machafuko miongoni mwa mataifa ya bara hilo.

Mwanadiplomasia huyo maarufu mno Afrika na duniano  alisema kuwa mabadiliko ya serikali kwa njia ambazo si za kikatiba yamepungua kwa kiasi kikubwa barani Afrika, kutengwa kwa baadhi ya makundi ya kisiasa kumekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mataifa mbalimbali.

Nadhani Afrika imefanya vizuri, angalau kwa sasa mabadiliko ya kiongozi kwa kutumia nguvu za kijeshi yamepungua kama si kumalizika.

Kama yapo, yamebaki katika makambi yao, lakini tunajaribu kutengeneza hali ambayo itawafanya waachane kabisa na dhana hiyo.

Iwapo kuna kiongozi yeyote ambaye atagoma kuondoka madarakani, iwapo kiongozi ataendelea kubaki madarakani kwa muda mrefu na uchaguzi unafanyika lakini ukiwa kama ‘changa la macho’ ili kuendelea kumpendelea aliyepo madarakani kumfanya aendelee kuwapo ofisini kwake kipindi hadi kipindi, kitendo hicho kinaweza kulazimisha kutolewa kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi au watu wataandamana mitaani kumshinikiza kuachia ngazi.

Hotuba hiyo inaelekea kuwalenga baadhi ya viongozi waliokuwa madarakani kwa muda mrefu mno, mmoja wapo akiwa ni Rais wa Uganda, Yoweri Museven ambaye amekuwa kiongozi wa nchi hiyo tangu Januari 29, 1986.

Rais Yoweri Museveni aliyetawala kwa kipindi hicho, alishinda tena uchaguzi wa mwaka huu uliogubikwa na utata kwa asilimia 60.75 (kura 5, 617, 503), huku mpinzani wake wa karibu, Dk. Kizza Besigye akipata asilimia 35.37 (kura 3, 270, 290), uchaguzi uliojaa vioja ikiwamo kuzimwa mitandao ya kijamii siku ya upigaji kura, wapinzani kuswekwa rumande na askari kupoka masanduku ya kura kwa dhamira wanazozijua wenyewe, akisahau alivyonyakua madaraka mara ya kwanza akitokea msituni.

Huko Sierra Leone, Serikali ya Rais Ernest Bai Koroma atakayemaliza muda wake mwaka 2018 licha ya kudai kuwa hana mpango wa kusalia madarakani, imeonekana kuwapo kwa kampeni kutoka kwa waliodaiwa kuwa ‘wananchi’ wanaompigia upatu aendelee kwa kuwa Ebola ilimega mwaka na nusu wa kasi ya maendeleo wakati ugonjwa huo ulipotikisa nchini humo.

Tayari serikali imetoa tamko kuwa iwapo Katiba ikibadilishwa bungeni kuiongezea muda itaridhia matakwa ya wananchi, kama ilivyotokea mwaka 2001 Bunge lilipomuongezea muhula Rais Ahmad Tejan Kabbah kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hotuba hiyo ya Annan pia imeonekana kuigusa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako hakuna uhakika wa kufanyika uchaguzi Novemba mwaka huu kama inavyopaswa, ikisemekana kuwa Rais Joseph Kabila anataka kuongeza kinyemela muhula wa tatu kinyume na Katiba kwani mwaka 2015 serikali ilishatamka kuwa uchaguzi unaweza kucheleweshwa kwa miaka minne zaidi hadi mwaka 2019, miaka mitatu zaidi ya muda uliopaswa kufanyika.

Ni wazi haitashangaza ikadai inahitaji mwaka mzima kufanya maandalizi na kutahamaki miaka mingine ya muhula wa tatu imetimia licha ya wapinzani kupinga vikali mchezo huo.

Nayo Rwanda imemuongezea muhula wa kuwa madarakani Rais Paul Kagame mwenye umri wa miaka 58 kupitia kura ya maoni ambapo atagombea tena muhula wake wa pili utakapokamilika mwaka 2017 ambapo muhula mpya wa miaka saba utamfikisha mwaka 2024.

Katiba hiyo iliyobadilishwa inatamka kuwa baadaye ukomo utakuwa mihula miwili isiyozidi miaka kumi, Kagame anaweza kudumu madarakani hadi mwaka 2034 akigombea tena na tangu mwaka 2000 aliposhika madaraka atatimiza takribani miongo mitatu unusu.

Mwenyewe Rais Kagame anakanusha kuutaka urais wa maisha ila anadai kuwa Wanyarwanda wanampendea mafanikio aliyowaletea baada ya mauaji ya Kimbari, ndiyo maana asilimia 98 ya watu milioni 6.16 waliopiga kura ya maoni wamekubali Katiba ibadilishe ukomo wa mihula.

Lakini Kagame huyo huyo ndiye anayeshutumu yaliyotokea nchini Burundi ambako tangu Rais Pierre Nkurunziza alazimishe muhula wa tatu wenye utata, wananchi wake wengi wamekimbilia nchi jirani kujinusuru na mauaji ya ovyo yanayorindima nchini humo. Lakini Serikali ya Burundi inakataa uingiliaji kati wa jumuiya ya kimataifa ikidai kuwa nchi iko salama ingawa makaburi ya halaiki yanazidi kugunduliwa, ingawaje hivi karibuni imelainika ikikubali mchakato wa usuluhishi huku harufu ya ubaguzi wa Kimbari ikianza kuugubika mzozo huo unaotishia marudio ya kilichotokea Rwanda miaka 22 iliyopita.

“Hakuna njia yoyote kati ya hizo ambayo inaonekana kuwa njia mbadala ya kidemokrasia, kwa uchaguzi au sheria za kibunge. Katiba na sheria za nchi lazima ziheshimiwe.

Annan, alisema kuwa kitendo cha viongozi kung’ang’ania madaraka, huwafanya wananchi kushawishika kirahisi kutoka kwa vyama vya upinzani katika harakati za kuichukia na kuikataa serikali yao.

Hali hiyo itawafanya kuungana na wapinzani katika harakati za kudai uchaguzi kwa nguvu zozote zile bila kujali madhara yake kwao na taifa lao kwa ujumla.

Annan alisema kwamba amekuwa kiongozi wa kwanza kuuambia Umoja wa Afrika kutokubaliana na Mapinduzi ya kijeshi ndani ya maeneo yao.

Kiongozi huyo alitoa wito huo katika mkutano wa viongozi wakuu wa Mataifa Huru ya Afrika uliofanyika mjini Lusaka, Zambia mwaka 2001.

Annan pia alisema kuwa suluhisho la matatizo ya bara hilo linatakiwa kutoka miongoni mwa wananchi na viongozi wa mataifa husika.

Hata hivyo, alisema kuwa bara hilo lazima lijenge uwezo wa kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kutatua matatizo yao, ikiwamo kugharamia mambo ya kifedha kwa vyuo vyao.

“Hatuwezi kupita huku na huko na kusisitiza kuwa tunataka kuwa huru, tunataka uhuru. Tunatakiwa kuongoza harakati zetu hizo ili wengine watusapoti. Sapoti hiyo inaweza kuwa kubwa na ya mafanikio ya hali ya juu watakapoona jinsi tulivyo makini na tunapambana vilivyo.

Mkutano huo ulikuwa chini ya Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, huku viongozi wengine waliohudhuria wakiwa ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Rais wa zamani wa Togo Faure Gnassingbe, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud na Rais wa Sudan Omar al Bashir.

Wengine ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, Rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae, Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano, Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya na Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles