31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wapinzani wanapoinasa migongeo ya Dilma Rouseff  

Dilma9HII ni mara ya kwanza tangu nianze kuandika safu hii kugusia mada moja mara mbili lakini si kwa marudio, bali ni mwendelezo wa mada iliyopata moto zaidi ya ilivyotarajiwa tangu sakata lilipoanza.

Kama tukinasibisha matukio yanayojiri nchini Brazil na maandalizi ya mlo basi wapinzani wa Rais Dilma Rousseff wameamua ‘kumpika’ kwa hatua mbalimbali, walimchemsha kisha wakamweka viungo na sasa wanamkaanga ili kumkamilisha awe asusa itakayotafunwa na mustakabali wa siasa tatanishi za Taifa hilo.

Kama umeanza kufuatilia hivi karibuni sakata hilo inawezekana umegubikwa na mvuto wa yanayojiri sasa lakini nikuhakikishie kuwa moto wa mambo hayo ulianza muda mrefu uliopita. Awali nilipoandika kuhusu sakata la Rais huyo mwanamama nililinganisha na kandanda, kwamba joto la sasa lilikolea zaidi baada ya Dilma kucheza migongeo na Rais mstaafu Luis Lula Da Silva sawa na kinachofahamika zaidi kwenye soka kama ‘kampa, kampa tena’.

Wapinzani wake wakiwamo wanasiasa wanaounda Serikali yake akiwamo makamu wake wakaungana kama safu ya mabeki, wakainasa migongeo (pasi) za Dilma na Rula wakidhamiria kushinda mechi kwa kufanya mashambulizi ya kustukiza.

Lakini baada ya Bunge la awali (Congress) kuidhinisha kwa kura zinazohitajika kuanzisha mchakato wa kushtakiwa na Senate (Bunge la juu) ili kumuondoa madarakani, Mwanamama Dilma ameapa kupambana huku akitamba kuwa ana nafasi ya kujitetea mbele ya Senate lakini pia akilaani hatua hiyo kuwa ya kidhalimu akiilinganisha na Mapinduzi.

“Kama ninayoshutumiwa kuhusika nayo yaliwahi kufanywa na viongozi waliopita na kuonekana halali iweje mimi nishikiwe bango kiasi hiki!?” Moja kati ya hoja anazotoa Rais Dilma katika kujitetea huku akijinasibu kuwa atatumia mbinu zilizomvusha katika kipindi cha mateso ya utawala wa kidikteta nchini humo kustahimili anachopitia sasa.

Kiutaratibu kama Seneta itapiga kura ya kukubaliana kuendesha mchakato huo wa kumuondoa madarakani, atalazimika kukaa kando kwa miezi sita wakati tuhuma dhidi yake zikichunguzwa na hilo likitimia inawezekana wakati wa ufunguzi wa michezo ya Olimpiki, atakuwa sio Rais kwa wakati huo.

Lakini yanayotokea sasa nchini humo yanakanganya kwa kiasi kikubwa, kutokana na wanaotaka Dilma ang’oke nao kuhusishwa na tuhuma zinazofanana na wanazomshutumu Rais wao.

Spika wa Bunge la Congress aliyesimamia kura za kuunga mkono kuanza kwa mchakato wa kumg’oa Rousseff, Eduardo Cunha, naye anatuhumiwa kwa ulaji rushwa hivyo inaelekea anatumia nafasi hii kuziba yanayomkabili kwa kushikia bango yanayomhusu Dilma.

Lakini kabla suala hilo kuanza kushughulikiwa na Senate Dilma alikuwa na nafasi ya kulikatia rufaa katika mahakama ya juu zaidi ambayo ilimtosa, hivyo sasa mambo yanapelekwa kikaangoni katika Senate na endapo akiwekwa kando makamu wake atashika wadhifa huo kwa muda wote mchakato utakapoendelea akiwa na mamlaka kamili ya kuteua mawaziri.

Hilo nalo ni neno ambalo linachangia mkanganyiko wa sasa katika siasa za nchi hiyo kwa kuwa Makamu wa Rousseff, Michel Temer, ambaye chama chake kinaunda Muungano wa Serikali iliyo chini ya Rais Dilma ni mpinzani wake anayeitamani nafasi hiyo hata kwa muda tu.

Ingawa naye ana tuhuma za kujibu na anahusishwa na yanayosababisha Dilma atake kung’olewa na mahakama ya juu imeliamuru Bunge la awali (Congress), lianze kumshughulikia pia ingawa kioja kingine pia kilichoibuka ni kuvuja kwenye mitandao ya kijamii hotuba ya Makamu huyo alipokuwa akifanya mazoezi ya kuhutubia kitambo atakapokabidhiwa madaraka.

Kama ni mchezo ndiyo kwanza umeanza maana ikiwa Dilma ataondolewa madarakani atakuwa Rais wa pili kukumbwa na kadhia hiyo, kwani Rais wa 32 wa nchi hiyo (Fernando Collor de Mello) aliyedumu toka mwaka 1990 hadi 1992 alijiuzulu wakati Senate likiwa katika mchakato wa kumuondoa.

Hata hivyo Rais huyo mwenye rekodi ya umri mdogo zaidi (miaka 40) kati ya waliowahi kushika madaraka nchini humo, aliyepatwa na hatia na kuzuiwa kushikilia uongozi hadi mwaka 2000 alikata rufaa kwenye mahakama ya juu na kushinda hivyo kumwezesha walau kugombea nafasi ya Useneta wa Alagoas aliofanikiwa kushinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles