25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

KOFI ANNAN: MSULUHISHI MTULIVU NA MAKINI

NA JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM             |         


KATIBU Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, (UN), Kofi Annan raia wa Ghana, aliyeaga dunia Jumamosi iliyopita baada ya kuugua kwa muda mfupi nchini Uswisi, alikokuwa akiishi alikuwa mwanadiplomasia, mpole, makini na mtulivu.

Anafahamika kama mwanadiplomasia ambaye  aliiongoza UN kimya  kimya na kumwagiwa sifa kwa sehemu kubwa kwa  kupandisha  hadhi  ya  taasisi  hiyo  kubwa  ya kimataifa   katika  siasa  za  dunia  wakati  wa  vipindi  viwili  vya uongozi wake kuanzia  mwaka  1997  hadi  2006.

Akiwa Katibu  Mkuu  wa  kwanza  kutokea  katika  eneo  la  Afrika  Kusini mwa  Jangwa  la  Sahara, Annan  aliongoza chombo hicho katika miaka migumu iliyoshuhudia mtengano na mgawanyiko kuhusu uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Irak.

Ni uvamizi, ambao pia ulionesha upande wa udhaifu wake, baada ya Marekani kukidhalilisha chombo hicho kwa kujiamulia kivyake nacho kikiangalia tu bila meno licha ya upinzani mkubwa wa wanachama wengi wa UN waliopinga vita hiyo.

Lakini pia ni vita iliyokuja kumwingiza katika shutuma za rushwa katika kashfa  ya  mafuta  kwa  chakula, programu ya UN iliyolenga kuisaidia Irak kwa kubadilishana mafuta.

Hiyo ni moja kati ya nyakati ngumu kabisa katika  kipindi  chake cha uongozi, kashfa ambayo mtoto wake Hani Yaman alihusishwa sana.

Lakini pia wakati wa miaka yake kumi kama Katibu Mkuu wa UN, Annan, mwanadiplomasia mwenye umbo dogo na ndevu za kijivu na mwepesi wa tabasamu mara nyingi alichukuliwa kuwa msuluhishi hodari, aliyezungumza kwa utulivu.

Alionekana hata kwa wale waliofanya naye kazi kwa karibu, kuwa mtu asiyejua hasira, ambaye hangeweza kufanya uamuzi peke yake—sifa ambayo inaakisi kile akizungumzacho, akipenda kutanguliza kauli zenye kuonesha upamoja katika upatikanaji wa uamuzi, mafanikio na au kufeli jambo fulani-‘sisi’.

Uwezo na hulka ya Kofi Annan wa kutekeleza yasowezekana, usuluhishi hodari na muwazi baina ya pande zinazopingana mara nyingi umetajwa kuwa moja ya nguvu zake. Lakini kwa upande mwingine wa shilingi kuna lililodhihirisha pia udhaifu wake.

Kabla hajawa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1997, Annan alitumikia kama mkuu wa idara ya kulinda amani ya chombo hicho chenye makao yake makuu New York nchini Marekani.

Katika wadhifa wake huo, alisimamia shughuli zilizofeli vibaya na aibu za kulinda amani nchini Somalia, Rwanda, na Bosnia.

Lakini hadi kifo chake nchini Uswisi Jumamosi ya wiki iliyopita, hakuwa tayari kukiri kuwa yeye binafsi au taasisi alizoziongoza zilipaswa kuwajibika na makosa hayo.

Hiyo ni pamoja na kuwa alizungumzia bila kuchoka hitaji la uongozi unaowajibika—“vichwa tulivu na uamuzi makini,” kama alivyopata kueleza wakati wa mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Aprili mwaka huu, moja ya matukio ya mwisho aliyoonekana hadharani wakati wa kuadhimisha miaka yake ya 80 ya kuzaliwa.

Hata hivyo, kama tulivyoona ana mengi ya kukumbukwa, mojawapo ni kuhesabiwa kuwa mmoja wa watu walioiokoa Kenya mwaka 2008 kiasi kwamba baadhi ya wabunge waligusia uwezekano wa kumpatia moja kwa moja uraia huku moja ya barabara kuu ikipewa jina lake mjini Nairobi.

Wakati wa machafuko ya mwaka 2007/2008 ya baada ya uchaguzi mkuu nchini humo, aliyekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, anakumbuka namna aliyekuwa Rais wa Kenya Mwai Kibaki alivyomsihi kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Kenya kipindi hicho, Moses Wetang’ula – kumsihi Kofi Annan asiondoke Kenya.

Hicho kiliashiria umuhimu wa Annan katika usuluhishi baina ya Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kufuatia machafuko yaliyoua watu 1,500 na wengine mamia kwa maelfu kukosa makazi.

“Nilipofika, Rais Kibaki akaniambia … kwanza, nimwambie Kofi Annan asiondoke kwani wakati huo mazungumzo yalivunjika. Na aliyeniletea ujumbe huo ni Moses Wetangula,” Kikwete alifichua hilo Oktoba 2015 wakati akilihutubia Bunge la Kenya.

Maneno ya Kikwete yanaoana na maneno ya Raila namna Wakenya walivyokuwa na imani na Annan: “… wakati Dk. Kofi Annan alipoamua kusitisha majadiliano, kulikuwa na kiza nchi nzima. Wakenya walikata tamaa. Hawakujua nini kitatokea,” Raila alieleza hilo mwaka 2008 wakati wa mjadala wa Sheria ya Mwafaka wa Kitaifa na Usuluhishi.

Hata hivyo, si wote wanaofurahishwa naye aliposhughulikia mgogoro huo, kwani kambi za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, ambazo kipindi hicho zilikuwa zimegawanyika baina ya Rais Kibaki na Raila zinamuona Annan kuwa sehemu ya waliochagiza kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Annan anaikumbuka siku yake ya kwanza kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa namna anavyoikumbuka siku yake ya kwanza shuleni.

Akiwa amezaliwa katika familia maarufu mwaka 1938 huko Kumasi, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ghana, baba yake alikuwa gavana wa jimbo la Ashanti chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza.

Ni kwa sababu hiyo, Annan alihudhuria shule za daraja la juu nchini Ghana, Uswisi na baadaye Marekani.

Annan alijiunga na UN akiwa na umri wa miaka 24 tu akianza kufanya kazi kama msimamizi katika Shirika la Afya Duniani (WHO) na kisha akawa mkuu wa watumishi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Baadaye alihudumu kama       Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) mjini Geneva, Uswisi na hatimaye kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, nafasi aliyoteuliwa kuishika mwaka 1993 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo Boutros Boutros-Ghali.

Katika nafasi hiyo aliwajibika upande wa masuala ya kulinda amani, akisimamia jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa lililokuwa na askari 75,000 duniani kote.

Kama mkuu wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Annan alipata kibano cha kwanza katika kazi yake mwaka 1994 wakati wanamgambo wa Kihutu wenye msimamo mkali walipowaua zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani.

Baadaye mauaji hayo yalitajwa  kama mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Annan alilaumiwa kwa kushindwa kutoa msaada wa kutosha katika nchi hiyo ya Mashariki mwa Afrika licha ya onyo la awali juu ya kuongezeka kwa ukatili lililotolewa na Romeo Dallaire, mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Kusita kwake kulitokana na ukweli kwamba Marekani na Ulaya zilionekana kuwa na maslahi madogo ya kujihusisha au kushiriki katika masuala ya Rwanda.

Annan aliomba radhi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa miaka 10 baadaye kwa kusema: “Jumuiya ya kimataifa imeshindwa kuinusuru Rwanda, na hiyo inatupasa daima kuwa na hisia za majuto, uchungu na huzuni ya kudumu.”

Mauaji ya kimbari ya Rwanda hayakusitisha kuendelea kukwea katika nyadhifa za juu kwa Kofi Annan katika Umoja wa Mataifa.

Alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu Desemba 1997, baada ya Marekani kushinikiza na hivyo akawa Mwafrika wa kwanza kutoka eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kuchukua nafasi hiyo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, alieleza kuwa hakutaka tu kufanya kazi za utawala kama mkuu wa Umoja wa Mataifa lakini pia alitaka kuunda upya siasa za kimataifa.

Ajenda yake ilikuwa ni pamoja na kupambana na umaskini wa kimataifa, kiwango cha kuongezeka joto duniani, na Ukimwi pamoja na ufumbuzi wa migogoro ya kisiasa.

Baadaye, alieleza kuhusu kusainiwa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya mwaka 2000 kuwa ni kielelezo kikuu cha kipindi chake akiwa ofisini.

Annan pia alisimama kama mwakilishi katika mgogoro wa Cyprus na Iran juu ya mpango wake wa nyuklia.

Alikuwa mkosoaji mkubwa wa mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Sudan wa Janjaweed katika jimbo la Darfur.

Mwaka wa 2001, Kamati ya tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Nobel ya Norway iliitambua michango ya Annan na kumtunukia yeye na Umoja wa Mataifa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Mwenyekiti wa Jopo la Oslo, Gunnar Berge, alisema kwamba Kofi Annan alikuwa mwakilishi bora wa Umoja wa Mataifa na pengine Katibu Mkuu aliyefanya kazi kwa ufanisi mkubwa kabisa katika historia ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema amesikitishwa sana na habari za kifo cha mtangulizi wake akimtaja kuwa alikuwa ni “nguvu iliyoongoza kwa mema”.

Naye mrithi wa Annan, Ban Ki-moon alisema; “kwa  ustadi  mkubwa  aliuongoza  Umoja  wa  mataifa  katika karne  ya  21 akielekeza  ajenda muhimu ambazo  ziliufanya  kuwa  na  mwelekeo  halisi  wa  amani, ufanisi na heshima  ya  utu duniani  kote.

Annan, ameacha mjane Nane na watoto Ama, Kojo na Nina, ambao walikuwa pamoja naye wakati umauti ulipomfika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles