24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kodi ya mishahara yashuka

mkuyaNa Waandishi wetu, Dodoma/Dar

WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amesema Serikali imeendelea na uboreshaji wa masilahi ya wafanyakazi ambapo kwa mwaka huu wa fedha imepunguza tozo la kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 12 ya sasa hadi asilimia 11.

Akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16 mjini Dodoma jana, Waziri Saada alisema hali hiyo inakwenda na dhamira ya Serikali kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi.

Alisema mshahara wa kima cha chini umeongezeka kutoka Sh 65,000 mwaka 2005 hadi kufikia Sh 265,000 mwaka 2014/15, ambayo ni asilimia 307.7.

Waziri Saada, alisema Serikali imeendelea kufanya marekebisho ya Mfumo wa Kodi ya Mishahara (PAYE) kwa kupunguza kiwango cha chini kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/07 hadi asilimia 11 mwaka 2015/16 ikiwa ni punguzo la asilimia 35.

Katika kuhakikisha Serikali inawaangalia wafanyakazi wastaafu, alisema katika mwaka 2015/16, wataongeza kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu wa Serikali kwa mwezi kutoka Sh 50,000 hadi Sh 85,000 sawa na ongezeko la asilimia 70.

“Serikali kwa kutambua mchango wa wazee wetu katika kujenga taifa hili, imedhamiria kuwalipa mafao ya kila mwezi, na kwa sasa Serikali imeanza kuandaa mfumo na utaratibu wa kuwatambua wazee wote nchini ili kupata idadi yao kamili na kuhakikisha mafao yanawafikia walengwa kwa wakati,” alisema.
MADENI YA MIFUKO YA HIFADHI NA WAZABUNI
Waziri Saada alisema Serikali imedhamiria kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa utaratibu wa kutoa hatifungani maalumu zisizo taslimu.
“Pia inatarajia kuendelea kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti ya Serikali ili kulipia deni linalotokana na wastaafu wanaolipwa mafao bila ya kuchangia kabla ya mwaka 1999,” alisema.
Akizungumzia hilo katika taarifa yake aliyosoma bungeni, Waziri Saada alisema madeni wanayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii, yalitokana na ulipaji wa mafao kwa wastaafu wenye utumishi wa kabla ya Julai Mosi, 1999, ambao hawakuchangia katika mfuko.
“Katika mwaka wa fedha 2015/16, Serikali imedhamiria kulipa madeni hayo kwa utaratibu wa kutoa hatifungani hizo maalumu zisizo taslimu na kuendelea kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti ya Serikali ili kulipia deni kutokana na wastaafu wanaolipwa mafao bila kuchangia kabla ya mwaka 1999.
“Hatifungani hizo zitakuwa na muda wa kuiva tofauti tofauti kwa kuzingatia mpangilio wa kuiva kwa dhamana nyingine za Serikali,” alisema.
Alisema katika miaka ya karibuni kumekuwa na malimbikizo ya madai mbalimbali yakiwamo ya madai ya makandarasi, wazabuni na watumishi.

Aliongeza kuwa hadi kufikia Aprili 2015, jumla ya madai ya Sh bilioni 692.2 yalilipwa, na Serikali inategemea kulipa Sh bilioni 200 zaidi kabla ya mwisho wa Juni 2015, ambapo kati ya fedha hizo, Sh bilioni 57.7 zimeshatolewa.

MIKOPO YA NJE
Waziri Saada alisema Serikali inatarajia kupata mikopo ya masharti nafuu na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo ya takribani Sh bilioni 2,941.5.
Alisema kufikia Aprili 2015 misaada na mikopo ya kibajeti iliyopokewa ilifikia Sh bilioni 408 sawa na asilimia 44 ya makadirio ya mwaka ya Sh bilioni 922.2.
“Fedha zilizopokewa kwenye mifuko ya kisekta ni Sh bilioni 289.5 sawa na asilimia 106 ya makadirio ya Sh bilioni 274.1 kwa mwaka. Kwa upande wa mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo, Sh bilioni 1,117 zilipokewa ambazo ni sawa na asilimia 64 ya makadirio ya mwaka ya Sh bilioni 1,745.3.
“Inakadiriwa kuwa hadi Juni 30, 2015 misaada na mikopo ya nje yenye masharti nafuu itafikia asilimia 70 ya lengo la mwaka na kutofikia lengo kunatokana na baadhi ya washirika wa Maendeleo wanaochangia GBS kutotimiza ahadi zao pamoja na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema.

SERIKALI KUKOPA DOLA MILIONI 800
Seikali imepanga kukopa dola za Marekani milioni 800 sawa na Sh bilioni 1.32 katika mwaka huu wa fedha kutoka kwenye vyanzo vya nje vya kibiashara ili kugharimia miradi ya maendeleo.
Waziri Saada alisema hadi Aprili 2015, Serikali imekopa dola milioni 300 sawa na Sh bilioni 514 kutoka Benki ya Maendeleo ya China (CDB) – kiasi hiki ni asilimia 39 ya kiwango kinachopaswa kukopwa kwa mwaka.
“Sera hizi za matumizi zimetekelezwa kwa mafanikio ya kuridhisha ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Bajeti ambapo utekelezaji wake utaanza Julai Mosi 2015,” alisema.

MATUMIZI YA SERIKALI
Waziri Saada alisema Serikali imetoa mgawo wa fedha za matumizi wenye jumla ya Sh bilioni 14,121.4 kwenye mafungu mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti.
Alisema fedha zilikuwa zimetengwa katika matumizi ya kawaida na mishahara ya watumishi wa umma na taasisi.
“Kati ya kiasi kilichotolewa, Sh bilioni 11,543.3 zilikuwa ni matumizi ya kawaida ikijumuisha mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi yenye jumla ya Sh bilioni 4,349.1.
“Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) Sh bilioni 4,467.9, Sh bilioni 2,726.3 za matumizi mengine na Sh bilioni 2,578.1 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles