Na Mwandishi Wetu, Songea
Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi amesema anaumia kuona baadhi ya wachezaji wa kigeni wanakaa benchi kutokana na kuruhusiwa kuchezesha nane pekee katika kila mechi.
Nabi amesema hayo leo Oktoba 18, 2021 mjini Songea wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC unataopigwa kesho kwenye dimba la Maji Maji.
Kocha huyo amesema kuna vitu wanaona havijakamilika licha ya kupata ushindi katika mechi zao za Ligi Kuu na kutokuruhusu bao, hivyo anataka kuongeza kitu ili kutimiza malengo ya klabu.
Amesema anataka kupata maoni kuhusu suala la Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), kutoruhusu wachezaji wote 10 wa kigeni kucheza katika mechi moja wakati msimu uliopita waliruhusiwa.
“Wameruhusu wachezaji wanane wakati dirisha la usajili limeshafungwa, ni kwamba umejiandaa kutumia wachezaji 10 na umewalipia kila kitu, sasa wakati umejiandaa hivyo vitu vyote inakuja kanuni inasema unachezesha wanane tu, hiyo inatuumiza.
“Mikakati ya kwetu imekuwa imegongana, tungejua tungenunua nane tu ili isingekuwepo usumbufu,” amelalamika Nabi.
Akizungumzia mchezo na KMC amesema lengo lao ni kushinda kila mechi iwe nyumbani au ugenini.
Akijibu juu ya suala la kuruhusiwa wachezaji nane pekee, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda amesema mchakato wa marekebisho ya kanuni wadau wa kwanza kuhusishwa ni klabu na Yanga ilituma mapendekezo yake yakajadiliwa.
“Suala la timu kusajili wachezaji 12 wa kigeni na kutumia nane katika kila mchezo, ni suala la kikanuni na mchakato wa marekebisho ya kanuni umechukua muda mrefu sana.
“Wakati mchakato unaendelea tulitangaza kuwa wadau na klabu zitume maoni, tunashukuru klabu ya Yanga ndio klabu pekee ilituma maoni ya mapendekezo ya kanuni, mapendekezo yote yaliyokuja yalijadiliwa katika vikao mbalimbali na vilivyohusisha viongozi wa klabu.
“Na hata maamuzi ya mwisho ya kwamba klabu zitaruhusiwa kutumia wachezaji nane tu wa kigeni ni maamuzi ambayo yalifanyika wakati usajili unaendelea,” amefafanua Boimanda.