26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

KKKT yawakumbuka watoto wanaoishi mazingira hatarishi Mwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Makao Makuu Arusha, limetambulisha mradi wa USAID Kizazi Hodari mkoani Mwanza ambao umelenga kuwafikia watoto 64,266.

KKKT inatekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa(USAID) ulioanza kutekelezwa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Manyara na Singida, Aprili Mosi 2022 na unatarajiwa kukamilika Machi 31, 2027.

Akizungumza jijini Mwanza Novemba 20, wakati akitambulisha mradi huo Kiongozi wa Mradi wa  USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kaskazini Mashariki, KKKT Makao Makuu Arusha, Dk. Godson Maro, amesema lengo kubwa la mradi  huo ni kuboresha afya, ustawi na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana walio katika maeneo ambayo yana maambukizi ya juu ya Virusi Vya UKIMWI.

Baadhi ya wadau watakaoshiriki kutekeleza mradi huo wakiwemo maafisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri za mkoa wa Mwanza wakijadiliana.

Dk. Maro amefafanua kwamba mradi huo ambao utagharimu Dola za Marekani milioni 27.4 kwa sasa unaendelea kutekelezwa katika mikoa ya Mara, Geita na Mwanza hivyo kufikia jumla ya mikoa nane.

“Katika Mkoa wa Mwanza mradi huu umelenga kuwafikia watoto 64,266 wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wameathirika au kuathiriwa na virusi vya UKIMWI kwa ajili ya kuwaunganisha na huduma za tiba ambazo zitawasaidia kufubaza virusi vya UKIMWI, tunawapa elimu ya kujitambua pamoja na huduma zingine jumuishi,” amesema Dk. Maro na kuongeza

“Walengwa wa mradi huu ni watoto wenye umri wa miaka 0 hadi miaka 17, pia tutatambua kaya maskini zenye uhitaji na kuziunganisha kwenye vikundi mbalimbali vya maendeleo  ili viwasaidie kuongeza kipato cha kaya waweze kuwahudumia watoto wenye maambukizi,”ameeleza Dk. Maro.

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka OR-TAMISEMI Mariam Nkumbwa, ametoa rai kwa watu wote watakaohusika katika kutekeleza mradi huo kuwajibika na kufanya kazi kwa kushirikiana ili malengo ya mradi huo yatimie kwa ufasaha.

Awali, akizungumza na wadau wanaotekeleza mradi huo ofisini kwake,  Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana alisema uongozi wa mkoa huo utashirikiana nao kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Faithmary Lukindo amesema mradi huo utasaidia watoto wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutokushindwa kwenda shuleni kutokana na kusumbuliwa na magonjwa nyemelezi kwa sababu watakuwa na afya nzuri kutokana na kufuata ufuasi mzuri wa dawa.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles