25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kizimbani kwa ubakaji, kujifanya mtoto wa CAG

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM 

AHMED Mudhihiri, amepandishwa kizimbani kwa mara ya pili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la ubakaji.

Mashtaka mengine ambayo yanamkabili Mudhihiri ni kujifanya mtoto wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mdogo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (Mwamvita Makamba).

Mudhihiri alifikishwa mahakamani hapo jana, lakini shauri lake liliahirishwa kwa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka hakuweza kufika mahakamani.

Akielezea mahakamani hapo mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Neema Moshi, aliiomba mahakama kutaja tarehe nyingine kwa ajili ya shahidi huyo kufika mbele ya mahakama. 

“Kutokana na shahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kufika mahakamani leo, naiomba mahakama itaje tarehe nyingine kwa ajili ya shahidi huyo kufika,” alisema Moshi.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Kiliwa alimtaka mshtakiwa kurudi tena mahakamani Juni 12. 

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka matatu.

Shtaka la kwanza, anadaiwa Julai 6, 2018 eneo la Hoteli ya White Sand iliyopo Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alimbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 26 raia wa Kenya. 

Katika shtaka la pili, mtuhumiwa alidaiwa Julai 6, 2018 katika Mkoa wa Dar es Salaam, alijidai kuwa yeye ni mtoto wa CAG kitu ambacho sio kweli. 

Na katika shtaka la tatu, anadaiwa Julai 6, 2018 eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, alidai kuwa yeye ni mdogo wa January Makamba (Mwamvita Makamba ) huku akijua anadanganya. 

Mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo, hata hivyo mahakama ilimtoa rumande baada ya kukidhi vigezo vya dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles