ERICK MUGISHA, DAR ES SALAAM
Mkazi wa Magomeni Mapipa Mariam Zuberi (21), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa tuhuma za kukutwa na noti 20 za bandia.
Akisomewa hati ya shtaka mbele ya Hakimu Lilian Silayo na mwendesha Mashtaka wa Serikali Ester Charles amedai mnamo Juni 27, 2019 eneo la Magomeni Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam bila kuwa na idhini ya mamlaka husika, alikutwa na noti 20 za bandia za sh 10,000 zenye thamani ya Sh 200,000.
Noti hizo zina namba za usajili GF4658564 noti 5, GF4658572 noti 4, GF4658567 noti 3, GF4658561 noti 2, GF4658562 noti 2, GF4658563 noti 1 na BK8169395 noti 1 huku akifahamu kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo mbele ya mahakama, huku upande wa Jamuhuri ukisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kesi kusikilizwa tena.
Hakimu Silayo amesema fungu la dhamana liko wazi kwa masharti kwa kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi zinazo tambulika kisheria na nakala ya vitambulisho vinavyotambulika na serikali ambao watasaini bondi ya Sh 500,000 kwa kila mdhamini.
Mshtakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa mpaka kesi yake itakaposikilizwa tena Septemba 26 Mwaka huu.