Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO
WATU wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Morogoro, kwa tuhuma za wizi wa mtoto waliyekabidhiwa kumpeleka Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mgolole.
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Theodora Mlelwa, alidai mbele ya Hakimu Agripina Kimanzi, kuwa watuhumiwa hao, Said Katalamu na mwenzake, Oswin Ngungantitu, wote wakazi wa Kitongoji cha Chekeleni, Tarafa ya Mikumi, Wilaya ya Kilosa, walitenda kosa hilo Septemba 26, mwaka jana, majira ya jioni.
Mlelwa alidai kuwa, watuhumiwa hao ambao ni wafanyakazi wa idara ya ustawi wa jamii wilayani Kilosa, walitenda kosa hilo baada ya kukabidhiwa mtoto huyo wa kiume kutoka Hospitali ya St. Kizito alikokuwa akitibiwa.
Kwa mujibu wa Mlelwa, watuhumiwa hao walifanikiwa kumuiba mtoto huyo baada ya kudai wanampeleka katika Kituo cha Mgolole ambako hawakumfikisha.
Alidai pia kwamba, mtoto huyo aliokotwa na Agripina Edga (43) akiwa na umri wa siku moja baada ya kutupwa pembezoni mwa reli akiwa amefungwa kipande cha sketi huku akiwa na damu, usaha, vidonda na mwili wake ukiwa umeshambuliwa na wadudu.
Watuhumiwa wote wawili walikana mashtaka yao na wako nje kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Agosti 23, mwaka huu.