NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina, amekitoza faini ya Sh milioni 10 Kiwanda cha Nyama cha Tanzania Meet Compay cha mkoani Dodoma, kwa kosa la kutokuwa na cheti cha mazingira pamoja na mfumo mzuri wa kutolea majitaka kiwandani hapo.
Mpina alichukua uamuzi huo alipokitembelea juzi ambapo alisema faini ya Sh milioni tatu ni kutokana na kiwanda hicho kukosa mfumo mzuri wa kutolea maji taka. Kutokana na hali hiyo, amekipa siku 14 kiwanda hicho kiwe kimelipa faini hiyo.
“Ninawapiga faini ya shilingi milioni saba kutokana na kutokuwa na cheti cha mazingira na shilingi milioni tatu ni kwa sababu kiwanda hakina mfumo mzuri wa kutolea maji taka ambayo hutumiwa na wananchi kwa ajili ya bustani na hivyo kuhatarisha afya zao,” alisema.
Pia Luhaga alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Leo Akonaay, kuanza utekelezaji wa kutunza mazingira, ikiwa ni pamoja na kutengeneza mfumo wa kutolea maji machafu.
Kwa upande wake, Akonaay alisema amepokea maagizo hayo na wako tayari kuyatekeleza kwa muda waliopewa.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kiwanda hicho huchinja ng’ombe 120 kwa siku kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi, huku wanaosafirishwa kwenda Omani wakiwa ni 30 hadi 50 kwa siku.
“Pia huwa tunachinja mbuzi 500 na kondoo 300 kwa ajili ya kupeleka Oman,” alisema.
Akonaay alisema mwaka jana walikuwa na wawekezaji 13 lakini kwa sasa wamebaki wawili kwa sababu ya kupanda kwa gharama za kodi na huduma za usafirishaji.
Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Hendson Alikatery, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema changamoto kubwa waliyonayo ni kutokuwa na mikataba pamoja na kushinda njaa kwa sababu mwajiri wao hatoi chakula kila siku, jambo ambalo linashusha morali yao ya kufanya kazi.