24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

KIU YA DAMU

peni

ILIPOISHIA…

Tayari mwendesha mashtaka aliandika kwenye karatasi. Aliandika maneno mawili makubwa kisha kunifuata.

“Hili ni ‘ndiyo’ na hili ni ‘hapana’,” alinieleza wakati akiyaonesha.

Kwa kuwa sikusoma, kumbukumbu ya kutapeliwa kwa mkataba wa kilaghai ilinijaa. Nilihofu kutapeliwa na mahakama pia kwa sababu ya ujinga wangu na upofu wa sheria. Nilikosa jibu hata uamuzi wa haraka. Baada ya nukta chache kupita ilibidi mwendesha mashtaka kurudia tena.

SASA ENDELEA…

 

“HII ‘ndiyo’ na hii ‘hapana’. Kama ni ndiyo tia alama yako ya vema hapa na kama hapana tia alama yako ya mkasi hapa. Umenielewa?” alizungumza kisha kunipatia kalamu.

Niliuelekeza mkono wangu hadi kwenye neno lililokuwa chini. Hapo nilitia alama ya vema. Kabla ya kuitua kalamu chini, niliparamiwa na kibao.

“Mwanaharamu. Kweli wewe zumbukuku. Hata kwa maelezo haya hutaki kuelewa. Sawa, ngoja nikufundishe kazi maana unatuchelewesha. Tutashinda hapa na shauri moja tu hadi jioni,” alifoka mwendesha mashitaka.

Aliondoka kwa kuzipiga hatua hadi kwenye meza yake. Alifika kisha kuketi. Aliichukua kalamu na karatasi kisha kuandika maneno kama aya nzima. Alinyanyuka kisha kunifuata pale nilipo kuwa kizimbani. Alinitazama kisha kusema:

“Sikiliza maneno haya kwa makini. Nikimaliza kusoma utatakiwa kukubali au kukataa. Kukubali inamaana utatia alama ya dole gumba chini yake. Ukikataa inamaana hutatia dole gumba lako. Tunaelewana?”

Kipindi hicho chote nilikuwa kimya nikimsikiliza kwa makini. Tayari aliizungushazungusha mkononi karatasi ile kisha kulisafisha koo lake tayari kwa kunisomea.

“Mimi Mbununu Mjuha Kilaza, kwa akili yangu timamu, nakubali au nakanusha tuhuma zote zilizotolewa juu yangu. Tuhuma hizi si za kweli au za kweli kwa shinikizo la nafsi yangu. Kwa maelezo haya, mimi nihukumiwe kadri mahakama iwezavyo,” alihitimisha mwendesha mashitaka kisha kunitazama.

Nilikuwa sielewi hata sikuamini sana maandishi yale. Aliniwekea katatasi kisha mkebe wa wino ambao ulikuwa umejaa.

Alinishika kono langu kisha kuuchovya ule wino. Aliuelekeza mkono wangu hadi juu ya karatasi ile yenye maandishi. Aliutua chini ya maandishi yale kisha kuugandamiza. Alama za dole gumba langu zilitabasamu pale kwa fahari. Zoezi lilikuwa limefika kikomo.

Hakimu na wote waliokuwa mahakamani pale wote pumzi zilizokuwa juujuu zilishuka. Wote walipumua kwa ahueni wakijua jambo lililowaweka muda wote lilipata tiba.

Nilistahili kuhukumiwa. Nilistahili kunyongwa hadi kufa kwani niliua kwa dhamiri yangu. Dhamira ya kuwaza, dhamira ya kujiandaa, dhamira ya kulinunua panga na kutembea umbali mrefu kisha kuua, tena kwa ukatili mbaya.

Kuua mtu baada ya mtu kwa dhamira ya moyo wangu. Kiu yangu ya damu ilipaswa kunitwaa kwa adhabu kali ambayo nilipaswa kujuta kisha kutoweka katika dunia hii kwa kunyongwa.

***

Mkanganyiko wa kisheria nilihisi kutokea hasa baada ya sauti yangu kushindwa kutoka mbele ya mahakama. Si sauti pekee, pia kutokujua kwangu kusoma pia lilikuwa pigo kubwa kwangu na mahakama katika uendeshaji wa shauri langu. Siku ya kusomwa shauri ilipoahirishwa nilitakiwa nilirudishwe gerezani kama mahabusu asiye na uhuru.

Nikiwa huko maisha yalikuwa si mwanana. Niliyoyategemea kutokana na fununu mbalimbali kutoka kwenye vikundi vya kahawa na wavutaji wa unga vilikuwa sahihi. Wapo walioolewa ingali jinsi zao ni za kiume na wapo waliooa ingali jinsi zao ni wanaume.

Yote hayo ni kujipumbaza. Hali ya gerezani ni ya ulimwengu wa pekee, hakuna haki, hakuna uhuru wala hekima miongoni mwa wafungwa. Wengi huenda kwa utashi wa mwili wakiweweseka na kuparamiana kwa vipigo na unyanyasaji.

Kila mfungwa au mahabusu mpya alikuwa sawa na kuku mgeni ambaye kamba miguuni kwake ilikuwa utambulisho. Kwa dokezo, nilipofika gerezani mambo mengi yalinishangaza.

Kupokelewa kwa kuvuliwa nguo hadharani, kubaki uchi wa mnyama mbele ya wenyeji. Upekuzi wa kila kona ulifanyika peupe pasipo kificho wala staha za utu.

Kingine ni vile biashara nyingi zifanyikazo katika dunia ya sheria na uhuru wa kuenenda kokote zilivyokuwa zikifanyika gerezani.

Watu huenda kwa haramu na halali. Sabuni na tumbaku ndicho kipimo halisi cha utajiri ambao sikuota wala kuuhisi. Mfumo wa biashara wa kubadilishana vyakula kama nyama na wali kwa kipande cha sabuni au funda la tumbaku ilikuwa fahari.

Nchi ya ajabu, gerezani watu huishi magenge magenge kwenye vijiwe kama mtaani wakiwa huru. Mbali na vurugu za maono, nilijionea matabaka ya kila aina yakiishi kwa kubaguana.

Wapo wenye misuli ambao ni wababe pia waonevu tayari kwa kuwanyanyasa wasio na maguvu kwa ufakiri. Wapo masikini wa haja, wasio na kipande cha sabuni mkononi, wasio nguo ya kuwasitiri wangali wakipepea na matambara mwilini mwao kwa miaka dahari.

Wapo matajiri wenye heri wapatao kila hitaji la msingi isipokuwa uhuru wa kutamba mitaani. Kwao chakula, mavazi na maisha ya anasa yote hujifariji nayo japo wako gerezani. Kuna jambo ambalo sikuwahi kuliota, nalo lilikuwa kuiona ndoo au beseni la plastiki lililopasuka likiwa limeshonwa kwa ufundi kwa kutiwa viraka.

Si kwa moto bali kwa nyuzi kama cherehani. Maajabu yalikuwa mengi na mengine nayamezea.

Itaendelea wiki ijayo.      

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles