27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kituo cha Fahari chapongezwa kwa umahiri katika ufundishaji

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Diwani wa Kata ya Gongolamboto, Lucas Rutainurwa, amekipongeza Kituo cha Elimu ya Awali cha Fahari kwa kuwa na walimu makini ambao wamekuwa chachu ya kuwatengeneza vyema watoto na kumudu kusoma, kuandika na kuhesabu.

Ametoa pongezi hizo leo Desemba 19, wakati wa mahafali ya sita ya wanafunzi wa darasa la awali yaliyofanyika katika kituo hicho kilichopo Gongolamboto.

Diwani wa Kata ya Gongolamboto, Lucas Rutainurwa akimpongeza mmoja wa wahitimu. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau

Katika mahafali hayo mmoja wa wahitimu, Nasri Chapozo ambaye pia ameibuka mwanafunzi bora kitaaluma amewashangaza wageni waliohudhuria sherehe hizo alivyosoma risala kwa niaba ya wenzake.

“Kwa namna mtoto huyu alivyosoma risala hii tena kwa lugha ya kigeni bila kubabaika huu ni uthibitisho tosha kwamba mna walimu makini ambao wanawapika watoto wetu vizuri,” amesema Rutainurwa.

Diwani huyo amesema pia lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu hivyo akawataka wazazi na walezi washirikiane na walimu.

“Serikali imahimiza sana juu ya umuhimu wa watoto kusoma hivyo lazima utiwe chachu na ninyi wazazi, maadili mema yanaanzia chini mtoto akiyakosa tabia na mienendo yake itakuwa mbaya.

“Mtoto anaweza kutoka katika mazingira tofauti nyumbani lakini akifika katika vituo kama hivi anayasahau kabisa kwani mambo mengine yanayofanyika nyumbani hayawajengei tabia njema watoto,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho ambacho kiko chini ya Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, amesema wanazo zana sahihi za kufundishia ambazo zinawawezesha watoto kuelewa yale wanayofundishwa.

Amesema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2014 mpaka sasa kina wanafunzi 128 na walimu tisa na tayari kimefungua tawi lingine lililopo Bangulo.

“Tumekuwa tukitoa elimu bora yenye malezi mema kwa watoto na kuifikia jamii inayoishi katika mazingira magumu, watoto wetu wako vizuri na hata wanapokwenda kufanya usaili katika shule mbalimbali hupata alama za juu,” amesema Mchau.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles