29.5 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kagera yakabiliwa na upungufu wa vyumba 250 vya madarasa

Na Nyemo Malecela Bukoba

Mkoa wa Kagera unakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 250 jambo lililosababisha Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia serikali ya Afrika Kusini kuchangia ujenzi wa madarasa 43.

 Upungufu huo umebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti wakati wa makabidhiano ya vyumba saba vya madara, vyoo 17 vyenye matundu 56 na nyumba za walimu mbili katika shule ya sekondari ya Mugeza iliyoko Manispaa ya Bukoba mkoani humo.

Gaguti amesema msaada huo uliotolewa na UNDP kupitia serikali ya Afrika Kusini ulitokana na athari za tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016 ambao umesaidia kupunguza upungufu wa madarasa unaoukabiri Mkoa wa Kagera kwa sasa.

“Msaada huo umekuja kwa wakati muafaka ambapo Januari tunatarajia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza tukiwa bado tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa,” alisema Gutia.

Naye Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kagera, Issa Mrimi alisema tetemeko hilo lilisababisha athari kwa viwango tofauti ikiwemo vifo, majeruhi na kubomoka kwa majengo na miundombinu ya barabara kwa wananchi 117,721.

“Kati ya wadau walioiwezesha serikali ya Mkoa wa Kagera katika hatua ya urejeshaji hali ya miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi ni pamoja na serikali ya Afrika Kusini kupitia UNDP ambao walitoa msaada wa bilioni 2.1.

Kiasi hicho cha fedha kilielekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu kwa kujenga wodi ya mama na mtoto, jengo la wagonjwa wa nje, madarasa 43, matundu ya vyoo 56, nyumba za walimu na watumishi wa afya tatu na Ofisi ya walimu moja kwa Halmashauri sita zilizokuwa zimepata athari za tetemeko hilo,” alisema Mrimi.

Issa alisema mradi wa wodi ya mama na mtoto iliyopo zahanati ya Buhembe Manispaa ya Bukoba haujakamilika kutokana na upungufu wa fedha za kumalizia mradi hivyo aliwaomba wafadhili hao ambao ni serikali ya Afrika Kusini na UNDP kuongezea zaidi ya Sh milioni 105.7 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Wakati huo Mkurugenzi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Matamwe Said aliwataka wakuu wa vyuo na shule za Msingi na sekondari waunde klabu au kamati za kukabiliana na maafa yote ikiwemo ya moto na elimu ya maafa ianze kusisitizwa katika mitahala ya masomo yao ili wanafunzi waweze kukabiliana na majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara shuleni na vyuo.

“Kutokana na janga la tetemeko la ardhi lililotokea 2016 mkoani Kagera lilisababisha nyumba za makazi ya watu 2,072 zilibomoka kabisa, nyumba 14,595 zilipata nyufa hatarishi na majengo 2,191 ya Umma yaliathirika kwa viwango tofauti.

“Uharibifu huo ulisababisha serikali kuweka kipaumbele katika kurejesha miundombinu ya kutolea huduma za afya na elimu kwa kuwa huduma hizo ni muhimu na zinatumiwa na jamii kila siku,” alisema Kanali Said.

Kanali Said alisema katika kurejesha huduma kwa jamii, miongoni mwa wadau walioisaidia serikali ni UNDP na serikali ya Afrika Kusini ambao wamejenga majengo ya kisasa katika shule na hospitali yenye uwezo wa kustahimili majanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles