28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wajumbe Kamati ya Fedha Igunga waonywa

Na Allan Vicent, Igunga

Wajumbe wa baraza la madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Igunga Mkoani Tabora ambao wameteuliwa kuingia katika Kamati ya Fedha wametakiwa kutobweteka kuwa wamepata ulaji bali watekeleze wajibu wao ipasavyo.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti Mpya wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucas Moga Bugota ambaye ni diwani wa kata ya Mbutu (CCM) katika kikao cha kwanza cha baraza hilo kilichofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa wajumbe wa kamati ya fedha hawapaswi kufurahia na kujiona kuwa wamepewa ulaji na kusahau kuwa kamati hiyo imebeba dhamana kubwa ya kuishauri halmashauri katika masuala yote ya kiutendaji.

Alibainisha kuwa wajumbe wa kamati hiyo wanapaswi kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa kwa kuwa watatoa ushauri na mapendekezo yanayobeba maslahi mapana ya halmashauri na wananchi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa mapendekezo hayo ambayo yataletwa mbele ya baraza yanapaswa kuwa na mtizamo mpana wa kimaendeleo na sio kuingiza maslahi binafsi hivyo akaonya kuwa mjumbe yeyote atakayezembea ataondolewa mara moja.

‘Serikali hii ya Chama Chama Mapinduzi chini ya Jemedari Rais Dkt John Pombe Magufuli haitaki ubabaishaji, ni ya hapa kazi tu, na mimi nataka kila mmoja awajibike ipasavyo katika nafasi yake, na si kufurahia posho tu’, alisema.

Bugota alisisitiza kuwa wananchi wanataka kuona fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa na thamani yake iendane na kazi iliyofanyika, si vinginevyo.

 Aliwataka madiwani wote kushirikiana ipasavyo katika kamati zao ili kuharakisha utekelezaji mipango mbalimbali ya halmashauri hiyo kwa manufaa ya wananchi wa kata zao.

 Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bi.Loyce Fumbuka (diwani wa kata ya Nyandekwa) aliwashukuru madiwani kwa kumchagua yeye na Mwenyekiti kuongoza halmashauri hiyo hivyo akawataka kuwa kitu kimoja ili kuharakisha maendeleo ya halmashauri hiyo.

Aliongeza kuwa changamoto zote zilizoko mbele yao kwa kipindi hiki ikiwemo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, uhaba wa walimu na mengineyo haviwezi kutatuliwa pasipo mshikamano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles