NA GEORGE KAYALA
MKONGWE wa muziki wa dansi nchini, John Kitime, ameukosoa muziki wa mwanamuziki mwenzake, Christian Bella, kwa madai kwamba una mapungufu mengi ya kiufundi.
Kitime alitoa hayo mwishoni mwa wiki, alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, iliyopo Sinza Kijiweni, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba, The African na Rai.
Kitime alisema mwanamuziki huyo ana sauti nzuri ya uimbaji, ila muziki wake umekosa vionjo, ndiyo maana unakosa uhai wa muda mrefu kama zilivyo nyimbo za zamani ambazo zinatamba mpaka sasa.
“Siku moja nilimsikia Christian Bella akisema atafanya mapinduzi makubwa kwenye muziki huu, ukweli ni kwamba hawezi kufanya lolole kwa kuwa muziki wake una mapungufu mengi, ingawa ana sauti nzuri ya kuimba,’’ alieleza na kuendelea:
“Kinatakiwa kisikike kila chombo, miaka ya nyuma ilikuwa hivyo, ndiyo maana mpaka sasa ukiusikiliza muziki huo hauchoshi masikioni,” alisema Kitime.
Msanii huyo aliongeza kwamba Watanzania wengi hawana elimu ya muziki, ndiyo maana wamekuwa wepesi wa kushabikia nyimbo zisizo na ubora kiasi cha kuwafanya wahusika waone wamefanikiwa, lakini baada ya muda huchuja, ndiyo maana kumbi nyingi za starehe kwa sasa zinapiga nyimbo za zamani kwa sababu zina utofauti mno na za sasa.