23.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

Kitanzi kipya watumishi wa umma

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

* Serikali yapeleka muswada bungeni kudhibiti posho,marupurupu holela

Na BAKARI KIMWANGA, DODOMA 

KITANZI kipya kwa watumishi wa umma. Ndivyo unavyoweza kusema kwa kuwa leo Serikali itawasilisha bungeni Muswada wa Sheria Mbalimbali unaolenga kubana zaidi watumishi wa umma.

Muswada huo, unaratajia kuwabana zaidi watumishi wa umma katika masuala ya posho na marupurupu ambayo walizoea kuyapata.

Mabadiliko hayo yamekuja mwaka mmoja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutoa ahadi ya kufanya marekebisho ya mishahara kwa watumishi wa umma ili kuweka uwiano sawa wa malipo yao.

Mabadiliko hayo, pia yatazihusu bodi mbalimbali za mashirika ya umma ambazo awali zilikuwa zikipanga posho na marupurupu kwa watumishi na sasa bodi hizo zitabaki na jukumu la kuangalia utendaji.

Muswada huo ambao umewekwa kwenye tovuti ya Bunge na kusainiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, unaeleza mabadiliko hayo ikiwamo sehemu ya tano inayopendekeza marekebisho katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 kwa lengo la kutoa tafsiri ya neno ‘recruitment Secretariat’.

Maneno hayo yametumika katika sheria, lakini hayakuwa yamepewa tafsiri.

“Kifungu cha nane kinapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi) kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma.

“Sehemu hii pia inapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A kinachozizuia taasisi za umma, wakala, bodi na tume zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi,” ilieleza sehemu ya muswada huo ambao unatarajiwa kuwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo.

Pamoja na hali hiyo, kifungu kipya cha 9B kinachopendekezwa, kinakusudia kuipa nguvu Sheria ya Utumishi wa Umma pale itakapokinzana na sheria nyingine kwenye mambo yanayohusu mishahara, posho na marupurupu ya watumishi.

“Muswada pia, unapendekeza kuweka kifungu kipya cha 32A kinachomtaka mtumishi kukamilisha taratibu zote za utatuzi wa migogoro ndani ya sheria hii kabla ya kutumia taratibu zilizoainishwa kwenye sheria nyingine.

“Inapendekezwa pia kukifuta kifungu cha 33 na kukirekebisha kifungu cha 34 ili kuakisi marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Waajiriwa ambayo yaliainisha Mfuko wa Fidia.

“Sehemu ya sita, inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma, sura ya 105,” inaeleza sehemu ya muswada huo.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa ili kupata ufafanuzi wa msimamo wa kamati yake kuhusu mabadiliko hayo ya sheria, alisema yuko kikaoni atumiwe ujumbe mfupi wa simu.

Hata hivyo, alipotumiwa ujumbe huo, hakuujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Aprili 5, mwaka huu, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema katika kipindi cha miezi 15 kuanzia wakati huo, mishahara mikubwa ya watumishi itapunguzwa na kuwa yenye uwiano.

“Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa, tunayo bodi ya mishahara iliyoanzishwa wakati wa Serikali ya awamu ya nne na jukumu lake kubwa ni kufanya mapitio ya mishahara mbalimbali na kuhakikisha mishahara ya watumishi wa umma haipishani sana.

“Katika hili, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana kupitia utumishi, hazina na msajili wa hazina ili kuangalia namna ya kulitekeleza agizo hilo,” alisema Waziri Kairuki wakati huo.

Alisema pia kwamba, mamlaka hizo hivi sasa zinaangalia mishahara ya taasisi mbalimbali na watumishi ili kuweza kubaini wale wanaolipwa zaidi ya Sh milioni 15 ni wangapi na itapunguzwaje ili iendane na matakwa ya Serikali.

Akizungumzia taasisi zinazozalisha kwa kiwango kikubwa na kuwa na uwezo wa kujiendesha, Waziri Kairuki alisema bodi ya mishahara hivi sasa ina jukumu la kuangalia uwiano baina ya mtumishi wa umma na mashirika ya Serikali.

“Unakuta mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa taasisi Y.

“Lakini, unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mara tano ya mtumishi Y, jambo ambalo si haki katika utumishi,” alisema.

Machi 30, mwaka huu, akiwa wilayani Chato, Mkoa wa Kagera, Dk. Magufuli alisema kuna watu wanalipwa mishahara mikubwa na kwamba wamekuwa wakiishi vizuri kuliko hata malaika na ni lazima washushwe ili waishi kama mashetani.

Hatua ya Rais Magufuli kupitisha panga na kuweka uwiano huo wa mishahara kwa watendaji wa taasisi hizo, unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa kwa watendaji.

Katika maelezo yake, Dk. Magufuli alisema anashangazwa na bodi hizo, kwani kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.

Ili kutatua tatizo hilo, alisema ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya kupunguza mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma wanaolipwa Sh milioni 36 hadi 40 kwa mwezi

“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya vikao Ulaya.

“Ninasema hapa kwamba, suala hili litaanza kushughulikiwa katika bajeti hivi karibuni. Yaani, kuna watu wanaishi vizuri kuliko hata malaika, hawa lazima tuwashushe waishi kama mashetani,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles