24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu: Serikali isiwaingilie viongozi wa dini

Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye (kushoto), Cleopa Msuya (wa tatu kushoto), Edward Lowassa (kulia) na viongozi wengine wa serikali, wakimsikiliza Askofu mteule wa Dayosisi mpya ya KKKT Mwanga, Chedieli Sendoro, wakati wa uzinduzi wa dayosisi hiyo mkoani Kilimanjaro jana.
Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye (kushoto), Cleopa Msuya (wa tatu kushoto), Edward Lowassa (kulia) na viongozi wengine wa serikali, wakimsikiliza Askofu mteule wa Dayosisi mpya ya KKKT Mwanga, Chedieli Sendoro, wakati wa uzinduzi wa dayosisi hiyo mkoani Kilimanjaro jana.

* Ataka isitumie nguvu kutatua migogoro ya  jamii

Na Safina Sarwatt, Mwanga

ASKOFU wa Dayosisi mpya ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chedieli Sendoro, amewataka viongozi  wa Serikali wasiwaingilie viongozi wa dini katika utendaji wao wa kazi.

Alisema utamaduni wa baadhi ya wakuu wa Serikali   kuwaelekeza viongozi wa dini nini cha kufanya usipewe nafasi kwa sababu unaweza kusababisha vurugu katika nchi.

“Kama ilivyo kwa kiongozi wa dini kutakiwa kutochanganya dini na siasa, iwe hivyo hivyo kwa kiongozi wa siasa kutojiingiza katika masuala ya dini zaidi ya kwenda  kuabudu,” alisema.

Akizungumza katika uzinduzi wa Dayosisi mpya ya Mwanga ya Kanisa hilo jana, Askofu Sendoro pia alishauri dini zote ziwe sawa mbele ya sheria na ziwe huru kutenda bila kuongozwa na mamlaka za serikali.

Dayosisi ya Mwanga imepatikana baada ya mgogoro wa zaidi ya miaka 20 ambao waumini wa Dayosisi ya Pare (Mwanga) wamekuwa wakipigania   kujitenga na ile ya Same.

Sendoro ambaye ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisis hiyo mpya,  alipendekeza iundwe  kamati za maridhianio kutafuta usuluhishi panapotokea msuguano wa makundi ya jamii badala ya serikali kutumia nguvu kutatua migogoro hiyo.

Alionya kuhusu matumizi makubwa ya nguvu katika kutatua migogoro, kwamba yanaweza kumomonyoa mshikamano wa taifa.

“Ili kuepusha matumizi ya nguvu kila  kunapojitokeza kutoelewana katika makundi mbalimbali, uwekwe utaratibu wa kuunda kamati mbalimbali za haki, amani na maridhiano katika ngazi mbalimbali na zisimamiwe na watu watakaochaguliwa na wanamakundi wenyewe.

“Wakutane na kuzungumza bila shinikizo la mtu yeyote. Mfumo huu ukitumiwa vizuri unaweza kuisaidia sana Serikali katika masuala ya amani, haki na kujenga maridhiano katika jamii,” alisema askofu huyo.

Askofu Sendoro alisema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na amani na uhuru mkubwa wa kuabudu na  hiyo ni moja ya nguzo muhimu iliyoliimarisha Taifa.

Kiongozi huyo wa Kanisa alisema  zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanaabudu kupitia dini mbalimbali na katika hao asilimia 50 ni wanachama wa vyama vya siasa.

Alishauri  suala hilo lisiwatenganishe bali wapewe uhuru wa kujadiliana huku masuala ya dini yakibaki nje ya utawala wa serikali.

“Tanzania ni nchi na pia Tanzania ni taifa  na taifa ni zaidi ya nchi…nchi inaweza kuongozwa na mtu mmoja lakini taifa hujengwa na
kuongozwa na timu ya watu wengi.

“Taifa lililojengwa na watu wengi na kwa muda mrefu, linaweza kubomolewa na mtu mmoja au kikundi kidogo iwapo wataachiwa na kufanya mambo yasiyo sawa.

“Ni maombi yangu kuwa taifa letu la Tanzania lililojengwa kwa muda mrefu na watu wengi liendelee kulindwa na kuwa na amani. Ili tufanikiwe katika hili tunahitaji uongozi wa pamoja bila kujali dini, itikadi, kabila au tabaka fulani,”alisema Askofu huyo.

Aliongeza kuwa Taifa imara ni tunda la kazi ya watu wa itikadi zote, dini zote na makabila yote hivyo ni vema mshikamano huo ukaendelezwa.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa siasa na serikali wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu,   Cleopa Msuya na Frederick Sumaye na Waziri Mkuuwa zamani, Edward Lowassa.

Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Angela Kairuki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles