30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kishindo fainali NMB MastaBata, Mil. 90 zapata washindi 

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MIEZI mitatu ya Kampeni ya ‘NMB MastaBata – Kivyako Vyako,’ iliyoendeshwa na Benki ya NMB, imefikia tamati Jumatano Machi 23 kwa wateja 30 kujinyakulia kitita cha Sh milioni 90 (sawa na Mil. 3 kila mmoja), hivyo kukamilisha kinyang’anyiro kilichobeba zawadi ya pesa taslimu Sh milioni 240.

Hitimisho ‘Grand Finale’ la kampeni hiyo, limefanyika NMB Tawi la Sinza jijini Dar es Salaam, kufikia ukomo kwa mchakato uliowanufaisha wateja 1,080, kati yao 1,000 wakijinyakulia Sh milioni 100 (sawa na Sh. 100,000 kila mmoja), huku 50 wakitwaa Sh milioni 50 (sawa na Mil. 1 kila mmoja) na 30 wa fainali wakishinda Sh milioni 90 hizo.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya NMB, Aikansia Muro  akibonyeza kitufe kuashiria kuchezesha Droo ya mwisho ya msimu wa tatu wa Kampeni ya NMB MastaBata Kivyako Vyako, wakati wa droo hiyo iliyochezeshwa katika Tawi la NMB Sinza Mori jijini Dar es Salaam jana. Katika Droo hiyo jumla ya wateja 30 walizawadiwa fedha taslimu Sh milioni tatu kila mmoja. Wa pili (kushoto) ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya Nmb, Filbert Mponzi, Balozi wa Kampeni hiyo, Masoud Kipanya na Meneja Mwandamizi kitengo cha Kadi, Manfredy Kayala.

Akizungumza kabla ya droo ya fainali hiyo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, alisema malengo ya kampeni hiyo, ambayo ni kuhamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu, yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kutamatika kwa NMB MastaBata ni mwanzo wa ujio wa kampeni nyingine.

“Tuko hapa kuhitimisha kampeni iliyoanza Desemba 2021, ikilenga kuhamasisha wateja kutumia kadi katika kufanya malipo. Matumizi ya pesa taslimu yapo, ila tunapaswa kuyapunguza kwa sababu za kiusalama. Tunatumia nguvu kubwa katika kuhamasisha wateja kutumia kadi za MasterCard kufanya malipo yoyote, bila kuwa na pesa taslimu.

“Kampeni hii ya miezi mitatu, imetoa zawadi za pesa kiasi cha Sh. Mil. 240, tumeshatoa Mil. 150 na leo tunaenda kutoa Mil. 90 kwa wateja 30. Hii inamaanisha kuwa NMB inatambua thamani ya matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu, kwa kuwazawadia wateja wanaofanya hivyo. 

“Pesa zilizotolewa kwa wateja ni kama motisha yetu kwao, kwamba wamefanya manunuzi kwa faida zao wenyewe, lakini sisi kama benki tukaona tuwazawadie katika kuchagiza matumizi yasiyohusisha pesa taslimu,” alisisitiza Mponzi mbele ya wanahabari na wageni waalikwa,” amesema Mponzi.

Balozi wa Kampeni hiyo, Masoud Kipanya (wa pili kulia) akipiga simu kwa mmoja kati ya wateja waliobahatika kushinda na kujinyakulia kitita cha sh. milioni tatu, wakati wa kuchezesha droo ya mwisho ya msimu wa tatu wa Kampeni ya NMB MastaBata Kivyako Vyako,  iliyochezeshwa katika Tawi la NMB Sinza Mori jijini Dar es Salaam jana. Katika Droo hiyo jumla ya wateja 30 walizawadiwa fedha taslimu Sh. milioni tatu kila mmoja. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya NMB, Aikansia Muro na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya Nmb, Filbert Mponzi, Kulia ni Meneja Mwandamizi kitengo cha Kadi, Manfredy Kayala

Aliongeza ya kwamba: “Kampeni hizi hazijakoma, zitaendelea na tutaendelea kutoa elimu kwa jamii itambue umuhimu wa mabadiliko, kwa sababu matumizi ya kadi ni rahisi, nafuu na salama zaidi. Kampeni imekuwa na mafanikio na kumekuwa na ongezeko la asilimia 10 la watumiaji wa kadi.

“Na kwa sababu kampeni kama hizi zitakuwa endelevu, basi wito wetu kwa Watanzania wasio na akaunti ni kufungua haraka iwezekanavyo na wale wateja wetu waendelee kuweka akiba ili kuwa wanufaika wa masuuhishi mbalimbali na kihuduma tunayotoa NMB,” aliongeza Mponzi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga, alipongeza aina ya ushirikiano baina ya NMB na Bodi yake, tangu kuanza kwa kampeni hiyo Desemba mwaka jana walipoenda kwao kuomba leseni ya kuendesha droo za kampeni hiyo.

“Pongezi kwenu NMB kwa kufuata taratibu, kuja kwetu kuomba leseni ya kuendesha kampeni hii na kila droo mkahakikisha kunakuwa na mwakilishi wetu. Kwa kipindi chote, hatukupokea malalamiko yoyote. Ilikuwa ni kampeni rahisi kwa mteja kushiriki, ile kufanya tu matumizi yako mwenyewe na kwa faida zako, unajikuta katika nafasi ya kuzawadiwa. 

“Na jambo la kufurahisha zaidi, idadi ya washindi ilikuwa ni kubwa mno, hivyo wanufaika walikuwa wengi. Mngeweza kubuni shindano dogo lenye kuwazawadia wateja wachache, ila mkaona hapana, muwafikie wengi zaidi, hili ni jambo la kupongezwa,” alimaliza Sengasenga, ambaye aliomba kuwe na muendelezo wa kampeni kama hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles