AYOUNDE, Cameroon
MGOMBEA urais wa upinzani nchini hapa, Maurice Kamto, ametaka kura katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita zihesabiwe upya na ameitka Jumuiya za Kimataifa kuchukua jukumu hilo.
Kwa mujibu wa matokeo ya kura hizo, Kamto alishika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia 14.23 ya kura nyuma ya Rais Paul Biya.
Katika madai yake hayo juzi, Kamto, ambaye alijitangazia ushindi siku moja kabla ya matokeo ya uchaguzi huo wa Oktoba 7 kutangazwa,anahoji kitendo cha kucheleweshwa wiki kadhaa kabla ya mshindi kutangazwa zilikuwa njama za serikali kuchakachua matokeo.
Alisema mbali na kuchelewa kutangazwa matokeo, pia kazi ya kuhesabu kura hizo ilijaa mizengwe na akasema kitendo cha Baraza la Katiba kumtangaza Rais Biya kuwa ndiye mshindi hakubaliani nacho.
“Kamwe hatuwezi kuyakubali matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Katiba,” alisema na kuongeza kwamba atapiga kampeni kwa amani dhidi ya matokeo rasmi.
Kamto (64) ambaye ni mwanasheria na kiongozi wa Chama cha MRC, aliwataka wapinzani wenzake kuungana naye kuendesha kampeini hiyo ya kupinga matokeo.