Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
MWANASIASA mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru (85) anatarajiwa kuagwa na kisha kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Kinjekitile Ngombare-Mwiru, ibada ya kuaga mwili wa baba yake itafanyika nyumbani kwake leo na mwili utaagwa katika viwanja vya Karimjee.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na wanasiasa mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe.
Nyumbani kwa marehemu jana, viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa walifika kuwafariji wafiwa.
Mbali na Mkapa, wengine ni Spika Mstaafu, Anne Makinda, Steven Wasira, Jaji Mark Bomani, Jaji Joseph Warioba, Nape Nnauye na wengine wengi.
Akizungumza katika msiba huo, msemaji wa familia, Balozi Ali Mchumo alisema wanatarajia kupokea wageni kutoka nje ya nchi ambao watashiriki mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe.
CHADEMA WASITISHA KAMPENI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametangaza kusitisha kampeni za mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Kinodoni, Salum Mwalimu zilizotarajiwa kufanyika leo ili kutoa nafasi kwa wananchama na viongozi wa chama hicho kushiriki shughuli ya mazishi ya Ngombale Mwiru.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa kumnadi Mwalimu katika eneo la Kinondoni kwa Manyanya Dar es Salaam jana, Mbowe aliwatangazia wananchama na wapenzi wa chama hicho pamoja na vyama vinavyounda Ukawa kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Karimjee ili kutoa heshima za mwisho kwa mwanasiasa huyo.
‘Napenda kuchukua nafasi hii kuwatangazia kuwa kesho (leo) hatutakuwa na kampeni Kinondoni, naagiza viongozi, wabunge, madiwani na wanachama wetu wa vyama vya Ukawa jitokezeni kwa wingi kwa utambulisho wenu tumuage Mzee Kingunge.
“Kama mnavyojua Mzee Kingunge alikuwa kada na mwanaCCM, lakini mwaka 2015 mzee huyu aliamini katika mabadiliko na kuamua kushirikiana na sisi kutafuta kura za Ukawa na ameondoka hajabadili msimamo huo,” alisisitiza Mbowe.
Kingunge alifariki dunia Februari 2, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alipokuwa akiendela na matibabu baada ya kung’atwa na mbwa wake Desemba 22 mwaka jana.
Kifo cha Kingunge kimetokea ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu mkewe, Peras Ngombale-Mwiru, afariki dunia Januari 4 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa.
Licha ya kuwapo kwa mijadala kadhaa kuhusu utaratibu utakaotumika wakati wa mazishi ya mwanasiasa huyo kutokana na kutokuwa mfuasi wa dini yoyote, familia yake imeeleza kuwa taratibu zote za kidini zitafuatwa kutokana na marehemu kurejea katika imani ya kikatoliki kabla ya kufikwa na mauti.
Mdogo wa marehemu, Enock Ngombale aliliambia MTANZANIA kuwa Kingunge alirejea katika misingi ya Kikatoliki alipokuwa akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Alisema licha ya kaka yake kutokuwa mfuasi wa dini yoyote, lakini alibatizwa alipokuwa mdogo na kupewa jina la Kaitano.
Wakati wa uhai wake Kingunge mwenyewe alisema kuwa alibatizwa na kufuata taratibu zote za Kanisa Katoliki isipokuwa hatua ya daraja takatifu la upadre.
“Ilikuwa ni wakati wa enzi za ukoloni, mkoloni Mwingereza, sikuwepo wakati wa mkoloni Mjerumani ….nilivyozidi kukua nilijikuta najiuliza sana maswali mengi mengi juu ya dhehebu la RC, najiuliza tangu darasa la kwanza hadi la kumi.
“Nilipochaguliwa kwenda sekondari Tabora akili yangu juu ya kuendelea kujiuliza maswali makubwa ikapanuka, niliendelea kujiuliza maswali ya msingi kuhusu imani ya dini, utatu mtakatifu.
“Niliuliza sana na nilipata matatizo nilipokuwa nauliza maswali kuhusu masuala hayo. Nilijiuliza kuhusu imani yangu, pia nikaacha kwenda kanisani” alisema Kingunge katika mahojiano ya na moja ya vyombo vya habari.
Wakati wa uhai wake, Kingunge aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo mkuu wa Mkoa, mbunge kwa vipindi kadhaa na uwaziri kwa nyakati tofauti.
Pia alishiriki katika harakati za kupigania uhuru kupitia Chama cha Tanganyika African National Union (TANU).
Ikumbukwe kuwa Kingunge alikuwa kiongozi na mwanachama mwenye ushawishi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kukihama chama hicho mwaka 2015 kutokana na kile alichokiita ukiukwaji wa katiba ya chama.
Alifikia uamuzi huo kutokana na kile alichokielezea kuwa hakufurahishwa na utaratibu uliotumiwa kumpata mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Pamoja na kukihama chama chake hicho alichokitumikia tangu kuundwa kwake mwaka 1977 hakujiunga na chama chochote cha siasa huku akisisitiza kuwa anaunga mkono mabadiliko.
Akiwa hospitali mapema mwezi uliopita, Kingunge alimweleza Rais Magufuli kuwa licha ya kuwa CCM ni chama chake alichokiasisi lakini amekihama.