24.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 30, 2023

Contact us: [email protected]

SARATANI TISHO KWA WATANZANIA

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


UGONJWA wa Saratani sasa ni tishio kwa Watanzania baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa takwimu zinazoonyesha kuwa kila mwaka karibu wagonjwa wapya 50,000 hugundulika kuwa na saratani za aina mbalimbali nchini.

Takwimu hizo zimeonyesha kuwa kati ya wagonjwa wapya wanaogundulika, 13,000 pekee sawa na asilimia 26 ndiyo wanaofika hospitalini kupata matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  alisema hayo jana kupitia taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma cha Wizara hiyo kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani yaliyofanyika jana.

“Wagonjwa walio wengi (takribani asilimia 70) hufika hospitalini kwa ajili ya matibabu wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa yaani hatua ya tatu na ya nne, hali hiyo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kupona maradhi haya,” alisomeka taarifa hiyo.

Taarifa ilisimeka zaidi kuwa takwimu za mwaka 2016/17 za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) zinaonesha saratani zinazoongoza nchini ni ya Shingo ya kizazi kwa asilimia 32.8, matiti asilimia 12.9, ngozi (Kaposis Sarcoma)  asilimia 11.7, kichwa na shingo asilimia 7.6, matezi asilimia 5.5, damu asilimia 4.3, kibofu cha mkojo asilimia 3.2, ngozi asilimia 2.8, macho asilimia 2.4 na tezidume asilimia 2.3.

“Ninatoa wito kwa kila mmoja wetu kupima ugonjwa wa saratani kwani inatibika endapo itagundulika mapema, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli itaendelea na jitihada za kuongeza uelewa  wa wananchi juu ya vyanzo mbalimbali vinavyosababisha saratani ili kila mmoja wetu aweze kujikinga.

“Vyanzo hivyo ni pamoja na mtindo wa maisha (Life Style) kama vile uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa (kula vyakula vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mboga mboga za kutosha), matumizi ya pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya na kutofanya mazoezi.

“Aidha, tutaongeza jitihada kuamsha ari na hamasa ya wananchi kupima saratani ili kujua hali zao sambamba na kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini,” alisomeka sehemu ya taarifa.

Aidha katika taarifa yake, Waziri Ummy alieleza kuwa mwaka 2017, Serikali imeongeza vituo 100 kutoka vituo 343 vilivyokuwa awali kwa ajili ya huduma za kupima na matibabu ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na ugonjwa huu.

“Vituo hivi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali) tumevipatia vifaa tiba na utaalamu ili kuwezesha wanawake wengi kupima saratani ya kizazi na matiti pamoja na kupata matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi papo hapo.

“Tumelenga kuwafikia wanawake milioni tatu nchi nzima ifikapo Desemba, 2018. Serikali inaendelea na jitihada za kusogeza huduma za matibabu ya Saratani (matibabu kwa njia ya dawa (Chemotherapy) na matibabu kwa njia ya mionzi (Radiotherapy) katika Hospitali za Rufaa za Kanda (Mbeya, Bugando na KCMC).

“Pia tunaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya Saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwa kuweka mashine mbili mpya za kisasa (Linear accerelators), ambazo zitasaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kupata  huduma za tiba ya mionzi sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100,” alisema,” ilisomeka taarifa.

Wakati huo huo Waziri Mwalimu kupitia taarifa yake hiyo alieleza kuwa kuanzia April, mwaka huu itatolewa chanjo ya kuwakinga wasichana kupata ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi  (HPV vaccine) kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 14.

“Niwaombe wazazi na walezi wenzangu tuwe tayari kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo hii, tunaweza, Ninaweza.

“Kwa pamoja tuwajibike kupunguza janga la Saratani Tanzania,” alitoa rai.

MTANZANIA jana lilifika katika viwanja vya ORCI na kushuhudia wananchi wakiendelea kupatiwa huduma ya uchunguzi wa awali dhidi ya magonjwa hayo.

Akizungumza na MTANZANIA, Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Dk. Maguha Stephano alisema uchunguzi huo ulianza Februari 3, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo na kwamba watu 110 wenye ulemavu wa ngozi (albino) kati ya 203 waliochunguzwa siku hiyo walikutwa ngozi zao zimeathiriwa na mionzi ya jua.

“Tulibaini ngozi zao zimeathiriwa mno sehemu ya kichwani, usoni na mikononi na kati yao wapo 25 ambao tumewagundua tayari wameanza kuonesha dalili za awali za saratani, wote hawa tumewapa matibabu na hivyo kuwaepusha kupata saratani ya ngozi,” alisema.

Dk. Maguha alisema katika uchunguzi huo wanawake tisa kati ya 162 waliojitokeza walikutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya shingo ya kizazi.

“Nao pia tumewapa matibabu na wawili kati yao tumewaita tena kesho (leo) ili tuwafanyie uchunguzi zaidi,” alisema.

Alisema wanawake sita kati ya 220 walikutwa na vivimbe katika matiti yao na kwamba wawili walionesha huenda vivimbe hivyo ni saratani.

“Hivyo hao nao tumewaita kesho (leo) ili tuwachunguze zaidi na tuwape tiba inavyostahili, kuna wanaume 98 ambao walijitokeza kuchunguzwa saratani ya tezidume watatu kati yao tuliwagundua  wana dalili za awali nao watakuja kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Imetosha, Henry Mdimu alisema jamii bado haina uelewa wa kutosha juu ya ugonjwa huo.

“Hasa wenye ulemavu wa ngozi, ndiyo maana tuliona vema kufadhili maadhimisho haya ili waje wafanyiwe uchunguzi wa awali na wale watakaokutwa na dalili za awali wapate matibabu mapema,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage alisema saratani ni ugonjwa ambao upo katika kundi la magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambayo kasi ya kuenea imekuwa ikiongezeka ikilinganishwa na kasi ya magonjwa ya kuambukiza.

“Lakini yanaweza kuepukwa ikiwa jamii itapata elimu ya kutosha kuhusu magonjwa haya, hasa kuzingatia mfumo mzuri wa maisha lakini pia kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

“Tunahitaji kuielimisha jamii ipasavyo na tunaona njia ya mitandao hususan simu za kiganjani ni rahisi zaidi kufikia kundi kubwa, hivyo tumepanga kutumia njia hiyo kutoa elimu kuhusu ugonjwa huu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,203FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles