MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
VIONGOZI wakuu wa vyama sita vya upinzani wamekutana visiwani Zanzibar kujadili na kutathimini mwenendo demokrasianchini.
Vyama hivyo vinavyoshiriki mkutano huo ni Chadema, CUF,NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, NLD na Chauma.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye aliyewaita visiwani Zanzibar viongozi hao kwa kikao cha siku mbili.
Jana, Maalim Seif aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kuwa anayo heshima kubwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa kikao hicho.
“Ni heshima kubwa kwangu na kwa CUF kuandaa na kuwa mwenyeji wa kikao cha kutathimini demokrasia yetu na kujitathimini sisi wenyewe kama vyama vya upinzani na mwelekeo wetu.
“Nawashukuru viongozi na watanzania mashuhuri waliopokea mwaliko wangu na kuhudhuria kikao hiki,”aliandika Maalim Seif.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa CUF, Salim Bimani aliliambia MTANZANIA kuwa viongozi hao watakapomaliza majadiliano hayo watazungumza na waandishi wa habari kueleza maazimio ya kikao hicho.
“Kesho (leo) au keshokutwa (kesho), tutazungumza na waandishi wahabari baada ya viongozi kumaliza majadiliano lakini kwa sasa hata mimi sijui kinachoendelea,”alisema Bimani.