30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kim Poulsen aisoma Simba Taifa

KimSAADA SALIM NA HUSSEIN OMAR, DAR

ALIYEKUWA kocha wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Kim Poulsen, kwa asilimia kubwa ndiye anatarajiwa kuwa mrithi wa Mwingereza, Dylan Kerr, kwenye kikosi cha Simba baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo MTANZANIA limezipata kutoka kwa kigogo mmoja wa Simba, mazungumzo kati ya Poulsen na uongozi wa klabu hiyo yamefikia pazuri na upo uwezekano mkubwa kocha huyo kurithi mikoba ya Kerr.

Chanzo hicho kililieleza gazeti hili kuwa, jana asubuhi Poulsen alikutana na viongozi wa juu wa Simba maeneo ya Mikocheni kwa ajili ya kujadiliana uwezekano wa kocha huyo raia wa Denmark kupewa mikoba ya Kerr aliyetimuliwa baada ya Kombe la Mapinduzi na Mganda, Jackson Mayanja kupewa majukumu ya timu hiyo kwa muda.

Imeelezwa kuwa katika mazungumzo hayo, Poulsen aliutaka uongozi wa Simba umpe muda kwanza ili aishuhudie timu hiyo ikiwa uwanjani dhidi ya JKT Ruvu jana kabla ya kuendelea na majadiliano yao.

Ili kujiridhisha na taarifa hizo, MTANZANIA lilimfuata kigogo mmoja wa Simba na kumuuliza kuhusu mazungumzo yao na Poulsen, ambapo bosi huyo alithibitisha kuwepo kwa mazungumzo kati ya klabu yake na Kim.

“Ni kweli tumekutana na Kim (Poulsen) na ametuambia kuwa anataka kwanza kuiona timu leo (jana), kisha kesho (leo) ndio tuendelee na mazungumzo,” alisema kigogo huyo wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Kigogo huyo aliongeza kusema kuwa hata kama wakifikia makubaliano na kocha huyo basi atapewa timu baada ya kumalizika kwa msimu huu hivyo makujukumu yake yataanza rasmi katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, chanzo hicho kimedai kwamba Simba inashindwa kumkabidhi Poulsen timu mapema kwa sababu kwa sasa timu hiyo haipo vizuri kifedha hasa baada ya kuvunja mkataba na Kerr ambapo wametakiwa kumlipa.

Poulsen jana alikuwa uwanjani kuishuhudia Simba ilipokutana na JKT Ruvu ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo mkali uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akiwa uwanjani hapo, Poulsen alionekana akiwa amekaa na kuteta na kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm kwa takribani dakika 45, hii ilikuwa kabla ya kuanza kwa pambano la jana.

Mbali na Pluijm, Poulsen pia alizungumza na kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa na Juma Mwambusi ambao pia walikuwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuangalia pambano hilo kati ya Wekundu wa Msimbazi na JKT Ruvu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles