30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Azam juu, Simba ya Mayanja safi

boccoOSCAR ASSENGA, TANGA NA MWALI IBRAHIM, DAR

TIMU ya soka ya Azam jana ilifanikiwa kurejea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwashusha wapinzani wao Yanga, baada ya kutoa kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Mgambo Shooting katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Matokeo ya ushindi wa jana yameiwezesha Azam kufikisha pointi 39 na kuwaacha Yanga nafasi ya pili wakiwa wamejikusanyia pointi 36, ambapo leo wanatarajiwa kushuka dimbani kuikabili Majimaji FC katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mgambo ambao waliifanyia mauaji JKT  Ruvu katika mchezo uliopita kwa kuilaza mabao 5-1, ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao dakika ya 17 kupitia kwa mchezaji wake Bolly Shaibu aliyeunganisha vyema krosi ya Azizi Gilla na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Azam, Aishi Manula.

Bao hilo liliwazindua Azam na kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa Mgambo ambapo dakika ya 22 mlinzi Shomari Kapombe alifanikiwa kuisawazishia timu yake kwa kumalizia pasi ndefu ya Ame Ally.

Wakati Mgambo wakitafakari bao hilo, walijikuta wakifungwa tena dakika ya 36 na Kapombe aliyetumia vyema makosa ya kizembe yaliyofanywa na kipa wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa langoni kwake.

Kwa upande wa Simba, waliocheza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu na kuendeleza machungu kwa maafande hao ambao walipokea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Mgambo Shooting katika mchezo uliopita.

Ushindi huo ambao ni wa pili mfululizo kwa kocha Mganda, Jackson Mayanja aliyepewa majukumu ya kukinoa kwa sasa, umerejesha matumaini kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo ambao walianza kukata tamaa kutokana na kupata matokeo yasiyoridhisha.

Matokeo hayo yameipa Simba nafasi ya kuendelea kung’ng’ania nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 33 ambapo imezidi kuwafukuzia vinara Azam pamoja na Yanga wanaoshika nafasi ya pili.

Dakika za mwanzo za mchezo huo, timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu kwa kila moja kusaka bao la mapema, lakini milango ilionekana kuwa migumu kwa pande zote.

Dakika ya 23, Emery Nimuboma wa Simba alishindwa kuipatia bao timu yake baada ya shuti alilopiga akiwa mbali na lango la JKT kutoka nje.

Kipindi cha kwanza kikosi cha JKT Ruvu kinachonolewa na kocha mkongwe, Abdallah Kibadeni, kilicheza kwa umakini mkubwa na kuwadhibiti washambuliaji wa Simba na kupunguza kasi ya mashambulizi langoni kwao.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 52 mwamuzi Martin Saaya wa Morogoro aliamuru penalti ipigwe langoni kwa JKT baada ya mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, kufanyiwa madhambi kwenye eneo hatari.

Kiiza aliyefunga mabao tisa msimu huu, alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti na kufikisha jumla ya mabao 10 sawa na Amissi Tambwe wa Yanga.

Bao hilo liliifanya JKT kufanya mabadiliko ya haraka dakika ya 55 ya kumtoa Issa Ngao na kumwingiza Amos Edward ili kukiimarisha kikosi hicho ambacho kilionekana kuelemewa.

Wakati JKT Ruvu wakijipanga kurekebisha makosa yao, Simba waliwaongezea machungu na kuongeza bao la pili dakika ya 61 kupitia kwa mshambuliaji wake Daniel Lyanga aliyewazidi maarifa mabeki na kumpiga chenga kipa na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, maafande wa Tanzania Prisons waliiadhibu Coastal Union kwa kuifunga mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kwa upande wao, Ndanda FC waliokuwa wamepania kulipiza kisasi cha kufungwa na Yanga bao 1-0 katika mchezo uliopita, waliifanyia mauaji Mbeya City kwa kuilaza kwa mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Stand United walifanikiwa kuendeleza ubabe katika uwanja wao wa nyumbani wa Kambarage, Shinyanga baada ya kuicha Toto African mabao 2-1.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles