NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Kim Paulsen, anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Mwingereza, Dylan Kerr, katika kikosi cha Simba ambacho kwa sasa kinanolewa na Mganda, Jackson Mayanja.
Kocha huyo raia wa Denmark alianza kuifundisha timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania kuanzia mwaka 2011 hadi 2012, alipokabidhiwa majukumu ya kuinoa Taifa Stars, baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Jan Paulsen.
Habari za uhakika ambazo zimelifikia MTANZANIA, zimeeleza kuwa awali Simba walikuwa wakimfikiria zaidi Kim, kabla ya kumleta Kerr na klabu hiyo ilimpa ofa ya kuja kuinoa timu hiyo, lakini ikashindikana.
Imedaiwa kuwa kwa sasa mpango wa kumnasa kocha huyo aliyekinoa kikosi cha Silkeborg IF kwa mwaka 2014/15, unaweza kuwa mgumu kwa kuwa sasa anakabiliwa na majukumu mengine, labda kama utatokea muujiza wa kuvunja mkataba wake alipo.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa, awali Simba walivutiwa na uwezo wa Kim, ambaye falsafa ya ufundishaji inafanana sana na Simba na pia anafahamu vizuri mazingira ya hapa nchini Tanzania, hivyo ataweza kuwamudu vema wachezaji wa timu hiyo.
“Kwa upande wangu ukiniuliza ni kocha wa aina gani anafaa kuifundisha Simba kwa sasa nitasema ni Kim, kwa sababu falsafa yake inafanana na Simba na pia yeye ni miongoni mwa makocha wanaofahamu vizuri mazingira ya kwetu,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, imedaiwa kuwa uongozi wa Simba unafikiria kuweka tangazo kwenye tovuti ya klabu hiyo ili makocha wanaotaka kuomba nafasi ya kuinoa timu hiyo watume maombi yao kwa kuzingatia vigezo vinavyotakiwa.
“Unaandaliwa mpango wa kuandaa tangazo la ajira ili makocha waweze kuomba nafasi ambalo litawekwa kwenye tovuti ya klabu na vigezo vinavyotakiwa vitabainishwa,” kilieleza chanzo hicho.
Aidha, chanzo hicho kimeeleza kuwa suala la kocha Hemed Morocco ambaye inadaiwa amependekezwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, halijakamilika na mazungumzo bado yanaendelea kati yake na uongozi.
“Suala la Morocco kupewa mkataba Simba si kweli, kwani uongozi bado unajadili ili kufikia uamuzi na pia hawezi kuwa kocha mkuu,” kilidai chanzo hicho.