27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

Lowassa: Wabunge, mameya mizigo kutimuliwa Chadema

Pg 1 jan 19Elizabeth Hombo na Arodia Peter

ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, amesema mameya na wabunge wa chama hicho wakishindwa kuwajibika watafukuzwa uanachama.

Lowassa alisema wabunge na mameya wa Ukawa, hususani wa Chadema wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wananchi waone tofauti kati yao na wale wa CCM walioongoza kwa muda mrefu Jiji la Dar es Salaam, lakini limeshindwa kupiga hatua.

Mwanasiasa huyo pia aligusia ubomoaji wa nyumba za mabondeni na sehemu zisizoruhusiwa, kwamba licha ya kutekeleza sheria, lakini lazima ufanywe kwa kuweka mbele ubinadamu.

Akizungumza katika kikao maalumu na mameya pamoja na manaibu wao kutoka manispaa za Kinondoni na Ilala, Lowassa alisema itakuwa ni aibu Dar es Salaam kuendelea kuwa chafu na kuzalisha ugonjwa wa kipindupindu.

Lowassa ambaye ni ni Waziri Mkuu mstaafu, alisema Kamati Kuu ya Chadema ilikwishatoa mwongozo kwa wabunge wake ambao watashindwa kuonyesha uwezo wa kufanya kazi za wananchi katika mwaka wa kwanza na wa pili wataondolewa ndani ya chama hicho.

“Hili ni agizo la Kamati Kuu kwamba mbunge na hata meya wakishindwa ku-perfom, ikipita mwaka mmoja au miwili hawajafanya chochote watafukuzwa kwenye chama.

“Chadema si chama cha kuendelea kuwa cha upinzani, tunajenga chama kinachojiandaa kushika dola muda wowote itakapopatikana fursa. Tunataka kuithibitishia dunia kwamba tunaweza kuongoza dola muda wowote zaidi ya CCM,” alisema Lowassa.

Pamoja na mambo mengine, Lowassa alitoa maagizo kwa mameya hao wa Ukawa kukusanya mapato na kuibua miradi mikubwa yenye masilahi kwa wananchi.

“Mkubaliane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili wakuu wa mikoa na wilaya wasiwazuie kufanya kazi zenu,” aliwaambia huku pia akiwasisitiza kuweka kipaumbele kumaliza uchafu na kuimarisha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mapato hayaonekani, kusanyeni mapato kuliko wakati wowote. Pia ondoeni sheria ya mhimili yaani wakuu wa mikoa na wilaya, hawa ni wavivu watawazuia katika spidi ya maendeleo yenu.

“Muondokane na sheria inayowazuia kukopa benki, kopeni benki na chagueni miradi ambayo inawagusa wananchi,” alisema.

 

MAMEYA WATOA SIRI

Aidha katika mkutano huo mameya hao kwa nyakati tofauti walifichua siri ya ushindi wao, huku wakimtaja Lowassa kwamba ndiye aliyewajengea uwezo wa kujiamini, kuwa wavumilivu na imara na hatimaye kuibuka washindi.

“Tunamshukuru sana kiongozi wetu Lowassa, alituandaa kama timu, alituweka kambini na akatujenga kisaikolojia, hivyo kambi hii ndiyo chachu ya ushindi wetu,” alisema Meya wa Ilala, Charles Kuyeko (Chadema).

Naye Naibu Meya wa Kinondoni, Jumanne Amir (CUF), alisema mafanikio yote ya Ukawa yametokana na Lowassa kuwajenga na kuwaondolea woga wa kuthubutu, hivyo hatua hiyo itawarahisishia kushinda kwa urahisi Uchaguzi Mkuu ujao 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles