KLABU ya Soka ya Azam FC imesema haina mpango wa kumfukuza kocha wa timu hiyo, Mwingereza Stewart Hall, kutokana na presha ya mashabiki wao ambao wanataka kuiga utaratibu zilionao klabu kongwe za Simba na Yanga.
Wiki iliyopita mashabiki wa Azam walitengeneza vipeperushi vya ‘HashTag’ na kusambaza mtandaoni, wakimtaka kocha huyo kuwaachia timu yao, wengine walifika mbali wakitaka Kocha Joseph Omog arudishwe.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mtendaji Mkuu wa klabu ya Azam, Saad Kawemba, alisema hawatamfukuza kocha wa timu hiyo, Hall, kutokana na presha za kuiga za mashabiki.
“Klabu yetu haiendeshwi kama zilivyo klabu za mchangani ambazo hazina utaratibu juu ya kuwalea makocha wao.
“Yanga na Simba ndio wenye utaratibu wa kuwafukuza makocha wao kila uchwao, utaona wanamleta huyu mwingine yupo njiani anasubiri, sisi hatuna mambo hayo,” alisema Kawemba.
Kawemba alisisitiza kwamba kocha huyo ni wa muda mrefu kwa maendeleo ya klabu, hawapo tayari kumfukuza hivi sasa kwa kuwa bado anafanya vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Msimu uliopita tulikuwa tunaongoza ligi kipindi kama hiki tukiwa na pointi 23, hivi sasa tupo nafasi ya pili tukiwa na pointi 36, hivyo utaona juhudi na maendeleo ya Hall.
“Ukiangalia tangu alipoichukua timu hii na makubaliano tuliyoyafanya katika vipengele vilivyopo kwenye mkataba, Hall anaendelea kufanya vizuri na hatuna sababu ya kumfukuza, tutakuwa wajinga kama klabu nyingine ambazo hazina utaratibu katika kufanya mambo yao,” alisema Kawemba na kuongeza kuwa klabu hiyo si ya wanachama kama ilivyo kwa klabu pinzani.
Kawemba alisema kwamba mashabiki wa klabu hiyo wanajulikana kwa kusajiliwa, huku akidai kwamba wanaotaka kocha afukuzwe si wanaotambulika kihalali na klabu.
Hall alisaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo Agosti mwaka jana, ameweza kuisaidia kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Shirikisho Afrika, inayotarajiwa kuanza Februari, mwaka huu.
Wakati huo huo, Azam inatarajia kuvaana na timu ya Mgambo JKT ya Tanga kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Akizungumzia mchezo huo, Hall alisema amekipanga kikosi chake kufanya vizuri kwenye mchezo huo baada ya sare waliyoipata katika mechi iliyopita.
“Mgambo itakuwa ni mechi ngumu, wamechukua pointi zao nyingi nyumbani, tayari wamechukua pointi dhidi ya Yanga jijini Tanga, hivyo kila kitu kitakuwa kigumu,” alisema Hall.