26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO WA PILI ACACIA AKAMATWA

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM


IKIWA ni wiki mbili tangu Makamu wa Rais wa Kampuni ya Acacia nchini, Deo Mwanyika, kukamatwa na vyombo vya usalama, jana kampuni hiyo imesema mmoja wa viongozi wake wa juu ambaye si raia wa Tanzania, amekamatwa.

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana ilisema mwajiriwa wake mwandamizi, anayefanya kazi na kampuni yake dada ya Pangea Limited,  “amezuiwa kuondoka Tanzania leo (jana) asubuhi, hati yake ya kusafiria ilizuiliwa na alishikiliwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kwa muda. Baada ya ufuatiliaji wa kisheria, aliachiwa na hati yake ya kusafiria ilirudishwa.”

Taarifa hiyo ilisema kuwa, tukio hilo ni moja ya ongezeko la matukio mbalimbali ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kupata misukosuko kutoka kwenye taasisi za kiserikali yaliyotokea ndani ya saa 48 zilizopita (tangu jana).

 

Kutokana na hali hiyo, ilisema inaendelea kuwasiliana na washauri wake wa kisheria na taasisi husika katika kuwasaidia wafanyakazi wao.

Taarifa hiyo, ambayo haikuweka wazi jina la kigogo wao aliyekamatwa, uraia wake wala bughudha ambayo wafanyakazi wao wameipata ndani ya saa hizo 48, ilisema kampuni hiyo inafuata sheria zote za Tanzania.

Ilisema pia kuwa, imekuwa ikisema kila kitu chenye faida kibiashara (commercial value), wanachozalisha na kwamba, imekuwa ikilipa mirahaba yote pamoja na kodi zinazotakiwa.

Taarifa hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu kampuni ya Barrick Gold Corporation ya Canada inayomiliki asilimia 63.9 za Acacia ya Uingereza kusema itakuja nchini wiki ijayo kufanya mazungumzo na serikali juu ya sakata la mchanga wa dhahabu (makinikia), ambalo ndilo chimbulo la mambo yote.

Majuma mawili yaliyopita, gazeti hili liliripoti taarifa ya Mwanyika kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola, kisha hati yake ya kusafiria na vifaa vyake vya mawasiliano kushikiliwa.

Mwanyika naye alikamatiwa Uwanja wa Ndege Dar es Salaam, ingawa haikuelezwa alikuwa anasafiri kwenda wapi.

Hata hivyo, msemaji wa Acacia alipoulizwa alisema: “Deo Mwanyika, Makamu wa Rais wa Acacia wa Masuala ya Shirika hajakamatwa wala hashikiliwi nchini Tanzania. Acacia inaendesha shughuli kwa uwazi na inakana tuhuma zozote za kuficha kiwango cha mapato ili kukwepa kulipa kodi stahili na inatoa ushirikiano kwa uchunguzi unaoendeshwa na Serikali ya Tanzania kuhusu tuhuma hizo,” alisema.

Juni 12, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alikabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Nehemiah Osoro.

Kutokana na hali hiyo, Kampuni ya Acacia ilieleza imesikitishwa na kushangazwa na matokeo ya ripoti hiyo, aliyokabidhiwa Mkuu wa Nchi.

Taarifa iliyotolewa na Acacia kupitia tovuti yake, saa chache baada ya ripoti hiyo kusomwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Nehemiah Osoro, ilisema kampuni hiyo imesikitishwa na ripoti ya kamati ambayo ni historia katika uchumi wa nchi hii na mambo ya sheria ya kusafirisha mchanga wa madini.

Siku hiyohiyo pia, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, Balozi Juma Mwapachu, alitangaza kustaafu nafasi hiyo baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili.

Taarifa iliyotumwa na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Acacia imemshukuru Balozi Mwapachu kwa utendaji wake na ushirikiano wake wote  alipokuwa mjumbe.

“Tunamtakia maisha mema,” ilieleza taarifa hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo, Bodi ya Acacia itabaki na wajumbe saba, wakiwamo wanne wakurugenzi na wasio wakurugenzi.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles