30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo BoT aachiwa huru

Pg 2NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Mifumo na Huduma wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Simon Jengo, aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya ofisi kwa kununua mashine 26 za kuharibu noti.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo Januari 30, 2012, chini ya Hakimu Ritha Tarimo, Wakili wa Serikali Fredrick Manyanda, aliyekuwa akisaidiwa na Ben Lincoln pamoja na Shadrack Kimaro.
Katika shtaka hilo, Jengo alidaiwa kutenda kosa hilo Juni 2005 na Desemba 2008, akiwa katika nafasi hiyo ambapo
alimshauri vibaya Gavana wa BoT katika ununuzi wa mashine hizo pasipo kujali mahitaji halisi ya benki.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hellen Riwa, alisema mshtakiwa ameachiwa huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kutaja kifungu cha sheria ambacho mshtakiwa alikiuka wakati wa kuagiza mashine hizo.

“Upande wa mashtaka ulidai kwamba mshtakiwa alikiuka sheria wakati wa uagizwaji wa mashine hizo, lakini
ulishindwa kubainisha ni kifungu gani cha sheria kilichokiukwa,” alidai.
Hakimu Riwa alidai pia imemwachia huru mshtakiwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na kubaini kwamba
mshtakiwa hakutoa uamuzi huo yeye binafsi, bali alishauriana kwanza na
wenzake kama timu.
“Upande wa mashtaka umeshindwa pia kuieleza mahakama idadi ya mashine ambazo zilihitajika kununuliwa na benki hiyo kwa wakati huo,” alidai.
Alidai kwamba, Mahakama imemwachia huru kwani katika kipindi ambacho alikuwa mtumishi wa benki hiyo alitunukiwa tuzo ya utendaji kazi bora na serikali.
Baada ya Hakimu Riwa kumaliza kusoma hukumu hiyo na kutoka nje, mshtakiwa ambaye naye alitoka nje alilakiwa na ndugu pamoja na jamaa zake waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya
kumpongeza.
Mshtakiwa huyo alikuwa nje kwa dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walisaini bondi ya
Sh milioni kumi kila mmoja kipindi chote cha kesi hiyo.
Jengo aliwahi pia kushtakiwa kwa kosa la kuhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara serikali ya shilingi bilioni 104 pamoja na wenzake, kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles