24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi lakana kunyang’anya vitambulisho vya kura

1NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekanusha kuwanyang’anya vitambulisho vya kupigia kura maofisa na askari wake na kudai kuwa kama kuna kiongozi anayefanya hivyo aache mara moja, kwakuwa ni kinyume cha sheria.
Jeshi limelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya askari wa jeshi hilo pamoja na polisi ya kulazimishwa na viongozi wao kutoa vitambulisho vya kupigia kura na wengine kudai kupewa
vitisho endapo watashindwa kuviwasilisha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano kwa Umma wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga, alisema jeshi hilo halijawahi kukusanya vitambulisho vya maofisa na askari hao na haliwezi kufanya hivyo kwakuwa utaratibu huo ni kinyume cha sheria.
“Hizi ni taarifa za upotoshaji na tulipozipata tulifanya mawasiliano na makamanda wa mikoa yote ili tujue limetokea wapi wakakanusha, lakini kama kuna mtu anafanya hivyo aache mara moja na kama mnamjua mleteni ili hatua za kisheria zifuatwe,” alisema Kanali Lubinga.
Alisema ofisi ya JWTZ makao makuu haijawahi kutoa maelekezo ya kukusanya vitambulisho vya kura na hakuna mtu ambaye anaweza kufanya hivyo bila maagizo, kwakuwa kila kitu kinachofanywa na viongozi wa kambi za jeshi nchi nzima kinakuwa ni maelekezo.
Alisema kazi ya viongozi wa jeshi ilikuwa kuwahimiza watu kujiandikisha ili waweze kupiga kura na si vinginevyo.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, jukumu la kuchagua kiongozi ni la mtu binafsi na hakuna maelekezo yanayotolewa kwa askari wa jeshi kwa kuwa wanajeshi hawatakiwi kuwa na wanachama wa chama chochote.

Aliongeza kwa sasa jeshi hilo linapitia katika kipindi kigumu kutokana na baadhi ya watu kufanya jitihada za kukichafua chombo hicho kwa kufanya upotoshaji.
“Sasa hivi kuna watu wamemaliza mafunzo wanajiita wanajeshi, naomba wananchi wawe makini kama ikitokea watu
wanachezea mfumo namna hii.

Waandishi pia mnapaswa kuwa makini na mambo haya ili tusije tukaingia kwenye gharika, tusichokane jamani, tupendane ili tutende yaliyopo mbele yetu,” alisema Kanali Lubinga.

Alisisitiza kuwa, JWTZ inafanya kazi kwa weledi, hivyo mwanajeshi anayekiuka huchukuliwa hatua za kinidhamu za kijeshi.
Wakati huo huo, Jeshi limekana wanajeshi wake kuhusishwa katika kashfa ya utoroshwaji wa meno ya tembo yaliyokamatwa nchini China hivi karibuni kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere (JNIA).
Badala yake, Jeshi hilo limesema hakuna mwanajeshi aliyeajiriwa katika uwanja huo.
“Hatuna mtu anayesafirisha meno ya tembo, uwanja wa ndege hatuna askari, kuna wastaafu walioajiriwa katika kampuni mbalimbali, hao huwezi kuwaita wanajeshi wetu kwakuwa hawapo katika mfumo wa jeshi wala hawapo katika payroll yetu (orodha ya malipo ya mshahara),” alisema Kanali Lubinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles