Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amemtumbua Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho nchini, Hassan Jarufu sababu akitaja ni kutoridhishwa na usimamizi wa zao hilo pamoja na upatikaji wa viwatilifu nchini.
Akizungumza juzi mjini hapa saa tano usiku, Dk. Tizeba alisema baada ya kuangalia mwenendo wa zao hilo na upatikaji wa viwatilifu na kwa jinsi linavyosimamiwa ameamua kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo.
“Baada ya kuangalia mwenendo wa zao la korosho linavyokwenda na upatikanaji wa viwatilifu na kwa jinsi linavyosimamiwa.
“Nimeamua kuchukua hatua ya kusitisha mkataba aliokuwa nao Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho, Hassan Jarufu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Tizeba alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,kufanya taratibu zinazohusika za kiutumishi kwa kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa mara moja.
Pia alimwagiza Katibu huyo kusitisha mara moja mkataba wa mtendaji huyo. Waziri Tizeba alisema ndani ya muda mfupi watatangaza mtu mwingine atakayekaimu nafasi hiyo.