31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

BABA MASOGANGE ASIMULIA ALIVYOONA  KIFO CHA MWANAWE

 

PENDO FUNDISHA (MBEYA) Na JOHANES RESPICHIUS


BABA mzazi wa aliyekuwa msanii wa video (Video queen) nchini, Agnes Gerald (Masogange), Gerald Waya, amesema kifo cha mwanawe alikifahamu kabla ya siku ya tukio baada ya yeye kuota ndoto iliyoashiria msiba utatokea ndani ya familia yake.

Amesema, ndoto hiyo ambayo alioneshwa msululu wa magari ukiwa nje ya nyumba yake ilimfanya kutokaa kwa amani huku nafsi yake ikiwa imejaa woga kwani aliamini ni kiashiria cha umauti kutokea ndani ya familia.

Agnes (29) alifariki dunia Aprili 20, 2018 akiwa Hospitali ya kwa Mama Ngoma alikokuwa akipatiwa matibabu.

“Ndoto hii iliniumiza sana kwani niliamini kuna jambo kubwa na la huzuni litatokea na hata ukiangalia ndoto inakuja na mwanangu Agnes akiwa amelala kitandani akiendelea kupatiwa matibabu juu ya ugonjwa wa kuishiwa damu uliokuwa unamsumbua,”alisema.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake jana, Mzee Gerlad, alisema kuwa taarifa ya msiba huo aliipata siku ya Ijumaa jioni kwamba mtoto wake amepoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika hospitali aliyokuwa amelazwa.

Alisema aliipokea taarifa hiyo kwa moyo wote kwani jambo alililolitabiri limetimia, hivyo hana budi kuhuzunika zaidi ni kumuachia Mungu.

Akielezea maisha ya awali ya mwanawe, baba huyo alisema kuwa kabla ya mwanawe kufikwa na umauti alipata nafasi ya kumwomba msamaha kwa yote aliyoyafanya ambayo yalikuwa yakimuudhi naye alimsamehe.

“Agnes kabla ya kwenda Afrika Kusini ambako alikamatwa na dawa za kulevya alifika nyumbani na kunieleza kwamba anasafiri lakini nilitumia nafasi hiyo kumsihi na kumtaka abadili mfumo wa maisha yake ambapo aliniahidi kufanya hivyo,”alisema.

Alisema, alipofika Afrika Kusini alimpigia simu na kumweleza kwamba amekamatwa na inasemekana amekutwa na dawa za kulevya jambo ambalo yeye marehemu alilipinga na kueleza kwamba amesingiziwa na baadhi ya wasanii wenzake lakini alimtaka baba yake asiwe na hofu.

Baba wa Masogange aliendelea kueleza kuwa baadaye alisikia mtoto wake huyo akiwa amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

“Nilimpigia simu na kutaka kupata ukweli wa tuhuma hizo aliniambia nisijali yatakwisha hadi siku ambayo mahakama inatoa hukumu yake alinieleza kwamba nisiwe na hofu na kwamba baada ya kutoka hapo yeye atakuwa mtoto mtiifu,”alisema.

Alisema, akiwa anaendelea na majukumu yake, marehemu alimpigia simu na kumweleza kwamba anajisikia maumivu makali ya mbavu lakini alimweleza kwamba anapaswa kwenda hospitali na asikae nyumbani.

“Wakati mtoto wangu anaendelea na matibabu, nilimpigia simu na kumtaarifu kwamba naumwa kifua lakini Masogange alinitaka niweke mikono kifuani ili aniombee na alipomaliza kufanya hivyo, nilimuuliza hali yake lakini aliniambia anaendelea vizuri kwani madaktari wanatarajia kumuongozea damu, huku akisisitiza nisiwe na hofu kwani anaamini atapona tu,”

“Lakini siku moja kabla alinipigia simu kwa kutumia simu ya mwenzake aliyemtambulisha kuwa ni kaka yake….na kubwa alilokuwa akitamka maneno yanayoashiria kuniaga…bye bye baba …kweli maneno haya yalinichanganya kichwa hadi siku ya Ijumaa napata simu kwamba amefariki dunia,”alisema.

Hata hivyo akimwelezea marehemu Masogange, mama mlezi Edina Mgogo, alisema Agnes aliondoka nyumbani kwa baba yake akiwa na umri kati ya miaka 14-15 alielekea jijini Dar es Salaam ambako alilelewa na shangazi yake, lakini siku zote baba yake alikuwa akitumia muda mwingi kumsihi mtoto wake abadili mfumo wake wa maisha kwani hayampendezi Mungu wala jamii.

“Namshukuru Mungu, Masogange alimwomba msamaha baba yake na alimwahidi kwamba atakuwa mtoto mwema na mwenye maadili na kwamba kabla ya mauti yake kumkuta tayari alianza kuboresha nyumba ya wazazi wake na kutuma Sh milioni 1.5 kwa ajili ya matumizi,”alisema.

VILIO VYATAWALA

Simanzi na vilio vilitawala jana katika viwanja vya Learders Club jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga mwili wa msanii huyo kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Utengule Mbalizi mkoani Mbeya ambako utazikwa leo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi, aliwataka waombolezaji kujiuliza baada ya safari yao ya hapa duniani ikifika tamati wataacha rekodi ya aina gani.

“Agnes ni ukumbusho maana kifo ni mawaidha tosha ni vizuri kila mmoja akajua hakuna maisha mengine zaidi ya haya, uwe maarufu kiasi gani mwishowe sote tutakufa hivyo lile jema ambalo unaweza kulifanya leo usisubiri kulifanya kesho. Swali kubwa tunaloachiwa na sisi tutamaliza safari yetu tukiwa na rekodi ya namna gani,” alisema Hapi

Katibu wa Msiba, Zamaradi Mketema, alisema Masogange ameacha mtoto mmoja Samia Sabri (11) ambaye anasoma darasa la saba.

“Masogange ameacha mtoto ambaye bado alikuwa na uhitaji mkubwa wa mzazi hasa ukilinganisha yupo darasa la saba na mwakani anatarajia kuingia kidato cha kwanza.

“Kwa hiyo kamati baada ya kufanikisha yote fedha iliyobaki Sh milioni mbili tumeiweka kwenye akaunti ya mtoto ili ikamsaidie kwenye masomo yake, pia tumeweza kumkatia bima ya afya ya miaka miwili,” alisema Zamaradi.

Naye mzazi mwenzake na Masogange, Sabri Shabani, alisema ili kumuenzi mama mtoto wake atamlea Samia katika maadili mema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles