27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

KIGEZO CHA USOMI HUANZIA KWENYE MATENDO YA MTU

Na Christian Bwaya

 

BILA shaka umewahi kukutana na mtu unayeamini ni msomi akifanya mambo usiyoyatarajia. Wakati mwingine unakata tamaa na kuhoji; “hivi huyu naye amesoma? Kama kusoma kwenyewe ndio huku, basi hakuna haja ya kusoma.” Pengine asiyekwenda shule angefanya hayo hayo wala usingeshangaa. Lakini kwa sababu elimu inatujengea matarajio fulani kwa mtu, unatamani kuona tofauti hiyo ikijidhihirisha katika maisha ya kawaida.

Tabia ya mtu aliyesoma, kwa mfano, inatarajiwa kuwa bora zaidi. Hapa tunazungumzia mambo madogo, lakini ya muhimu, kama vile heshima kwa watu, uwezo wa kuvumilia mawazo tofauti na namna anavyoweza kuwasilisha mawazo yake. Hivi ni baadhi ya viashiria vinavyotumiwa na jamii kupima ikiwa ni kweli mtu ameelimika.

 

Ingawa ubora wa elimu ya mtu unaweza kupimwa kwa uwezo wake wa kuona na kutatua matatizo yanayoikabili jamii, mara nyingi jamii huangalia mambo yanayogusa utu wa watu. Tunu kama vile uadilifu, uaminifu, kusema kweli na unyenyekevu zinachukuliwa kwa uzito mkubwa wakati mwingine kuliko fani halisi. Mtu aliyesoma na bado akawa tapeli, mlaghai, mwenye majigambo, mlevi, mzinzi, hufanya watu wawe na wasiwasi na elimu yake. Mara zote mtu anapoonesha tabia hizi, watu watajiuliza; “Elimu ina faida gani kama mtu anafanya mambo ya kijinga kama haya?” Kwa mukhtadha huu, mabadiliko ya maisha ni kipimo muhimu cha ubora wa elimu aliyoipata mtu.

Kadhalika, jamii inaamini mtu aliyesoma lazima aweze kumudu maisha yake. Usomi wake ni lazima uende sambamba na kuboresha mtindo wake wa maisha. Huwezi, kwa mfano, kusema umeelimika na bado ukabaki kuwa masikini. Katika macho ya jamii, umasikini ni kiashiria cha mtu aliyeshindwa kuelimika. Elimu lazima ikusaidie kutuia maarifa yako kujipatia/kujiongezea kipato. Unapokuwa na elimu kubwa lakini huna uwezo wa kubadili changamoto zilizopo kwenye jamii kuwa fursa, watu wanakuwa na wasiwasi na wewe. Wakati mwingine, hali hiyo inafanya jamii iwabeze wasomi kwamba wamepoteza muda mwingi kujifunza mambo ambayo yameshindwa kuwasaidia kuboresha maisha yao wenyewe. Kwa mujibu wa jamii, kushindwa kumudu maisha yako kunaweza kuwa kiashiria cha elimu isiyokidhi haja.

 

Inawezekana ni kweli jamii ina mtazamo hasi dhidi ya elimu. Tunafahamu, kwa mfano, lipo wimbi la kujaribu kuifanya fedha iwe ndio kipimo cha heshima ya mtu. Lakini ni kweli pia kwamba wasomi wenyewe –kupitia namna wanavyoonekana kupitia mchango walionao kwa jamii –ndio  waliochangia kukuza mtazamo hasi uliopo kwa jamii dhidi ya elimu. Kwa kuwa matokeo ya elimu ni sharti yaiguse jamii, ni dhahiri jamii isipoguswa na matokeo hayo, maana yake ni kwamba wasomi wameshindwa kufanya wajibu wao.

 

Mojawapo ya sababu zinazofanya elimu ishindwe kuwa na manufaa kwa watu na jamii kwa ujumla ni msisitizo wake kwenye eneo moja tu la taaluma. Tangu mwanafunzi anapoanza darasa la kwanza mpaka chuo kikuu anatarajiwa kuelimika kwa kipimo cha kufaulu mitihani. Mzazi anategemea mtoto arudi nyumbani na cheti chenye alama za juu. Wakuu wa elimu wanalenga kupandisha ufaulu wa mitihani. Mwalimu naye kwa upande mwingine, hana namna nyingi zaidi ya kufanya kazi ya ziada kufikia matarajio hayo kwa kuhakikisha mwanafunzi anafaulu kwa kiwango cha juu.

 

Athari mojawapo ya mtazamo huu finyu wa elimu ni kusahaulika kwa maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya binadamu. Siha nyingine muhimu zinazokuza utu na utimamu wa binadamu kama vile nidhamu, maadili, bidii ya kazi, uaminifu, afya ya akili na mwili, stadi za maisha na ukuaji wa kiroho hazipewi nafasi inayostahili. Mitalaa yetu inabaki kutushinikiza kuvielewa vitu na pengine kukuza uwezo wa kudadisi mambo kuliko kujielewa na kuwa binadamu timamu. Tunafikiri maarifa ya vitu ndio msingi wa maendeleo. Matokeo yake, wanafunzi wanapata alama A darasani lakini hawana nidhamu itakayowasaidia kufanikiwa kwenye maisha.

 

Ni vema tukitambua kwamba ufaulu mzuri usiokwenda sambamba na kujengwa kitabia hauwezi kuwa na manufaa ya maana. Tunahitaji kuweka msisitizo katika kukuza maeneo yote muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi. Tujenge mfumo thabiti wa kuwalea vijana kimaadili na kiroho ili maarifa wanayoyapata yawasaidie kuwa binadamu wenye tija kwa jamii. Sera zetu za elimu, kadhalika, zisiishie kuelimisha akili za vijana wetu na kuwaacha hawajitambui wao ni nani na nafasi yao katika jamii. Vinginevyo, elimu itabaki na kazi ya kumwandaa mtu atakayesubiri kuajiriwa ili apate fursa ya kutumia maarifa yake kuiba na kujiletea manufaa yake

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles