NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI mpya kutoka nchini Zambia Obrey Chirwa amewasili jijini Dar es Salaam jana tayari kwa ajili ya kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga kwa ajili msimu ujao na michuano ya kimataifa.
Chirwa aliwasili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo inasemekana Yanga, ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho wamelazimika kulipa Shilingi milioni 200 kwa nyota huyo wa FC Platinum ili kuweza kupata saini yake.
Mshambuliaji huyo alijiunga na FC Platinum misimu miwili iliyopita ambapo mwaka jana alikwenda kucheza soka la kulipwa klabu ya Horbo IK ya Dermark ila baada ya kutovutiwa na maslahi aliamua kurejea katika klabu yake.
Yanga ambao wapo nchini Algeria kwa ajili ya mechi yake ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, dhidi ya MO Bejaia itakayochezwa kesho, huku uongozi ukiwa na matumaini makubwa
kuwa Chirwa atafanya vizuri kama walivyofanikiwa wachezaji wenzie wa zamani wa FC Platinum Donald Ngoma na Thabani Kamusoko.