CLARA MATIMO Na MASYENENE DAMIAN
KICHOCHO cha tumbo hushambulia viungo vya uzazi vya mgonjwa na kusababisha ugumba, saratani ya kizazi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Hayo yalielezwa jana na watafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kituo cha Mwanza, Dk. Godfrey Kaatano na Dk. Julius Siza.
Walikuwa wakizungumza na MTANZANIA juzi kuhusu athari ambazo mgonjwa wa kichocho anaweza kuzipata endapo atachelewa kupata matibabu.
Kwa mujibu wa watafiti hao, kichocho cha tumbo huenea zaidi katika maeneo ambayo shughuli za uchumi hufanyika katika maji.
Waliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi nchini kuwa ni ya ukanda wa Ziwa Victoria ambako aina zote mbili za kichocho cha tumbo na mkojo hupatikakana huku kiwango cha maambukizi kikifika hadi asilimia 100 katika baadhi ya maeneo.
Dk. Siza alisema mayai ya vijidudu hivyo yana ncha kali ambazo hutoboa mirija ya uzazi na kuharibu kizazi kusababisha ugumba kwa mwanamke.
Alisema kwa mwanaume husababisha majeraha ambayo husababisha vimelea vya Ukimwi kujipenyeza kwa urahisi wakati wa kujamaina.
Dk. Kaatano, alisema mtoto akiugua kichocho cha tumbo au kichocho cha mkojo husababisha madhara ikiwamo mahudhurio mabaya shuleni, kudumaa ubongo, ukuaji hafifu na hata akiwa mkubwa hawezi kuzalisha kwa tija.
“Mkoa wa Mwanza uko katika ukanda wa ziwa Victoria ambako kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa kichocho ni cha juu.
“Katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na mradi wa SCORE katika shule 150 za mkoa huu, watoto wa shule wapatao 27,926 wenye umri kati ya miaka 6-12 walipimwa na wastani wa kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 60,” alisema Dk. Kaatano.
“Katika kujikinga na ugonjwa huu tunahimiza zaidi tiba kinga kwa kutumia dawa aina ya Praziquantel na Albendazole na chanjo kwa watoto na wanafunzi kwa sababu ndiyo waathirika wakubwa.
“Lakini tiba hiyo haizuii maambukizi ya kichocho, elimu ya afya, matumizi ya maji safi na salama, matumizi sahihi ya vyoo na kudhibiti konokono ni muhimu,” alisema Dk. Kaatano.