23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali itoe elimu kwa wafanyabiashara wa korosho

korosho-1024x650

NA FLORENCE SANAWA,

SERIKALI imekuwa ikiweka kipaumbele kuwasaidia wakulima wa korosho mkoani Mtwara ili waweze kunufaika na zao hilo.

Aidha, imekuwa ikijaribu kuwapiga vita wafanyabiashara wachache wanaowarubuni wakulima na kuwauzia korosho kwa bei ndogo, hali ambayo inawaongezea umasikini.

Hatua hii inaonekana kugonga mwamba baada ya wakulima wengi kuishi katika mazingira magumu, huku uchumi wa familia zao ukiwa chini, hatua ambayo inawalazimu kutumia njia mbalimbali kuficha korosho mithili ya bangi na kuiuza ili waweze kupata fedha ya chakula.

Uuzwaji huo holela umeonekana kukithiri katika maeneo mbalimbali, kiasi kwamba korosho imekuwa kama bidhaa ya magendo.

Kwa kutambua kuwa korosho ndilo zao pekee linalolimwa mkoani Mtwara na linaloingiza mapato makubwa kwa Serikali, hali ambayo imeilazimu Serikali kuwapunguzia mzigo mkubwa wa tozo wakulima wa zao hilo ikiwemo kuwapa pembejeo kwa mfumo wa ruzuku.

Katika miaka ya hivi karibuni, mavuno yamepanda kwa kasi hali inayoashiria kuongezeka kwa mapato katika halmashuri za mkoa huo kutokana na ushuru unaolipwa na wakulima wa zao hilo.

Ikumbukwe kuwa zao hilo ni uti wa mgongo kutokana na mkoa huo kuongoza katika ulimaji na uvunaji, huku halmashauri zikisimama na kujiendesha kutokana na ushuru unaolipwa na wakulima wa zao hilo.

Hata hivyo, kumeibuka mtindo wa usafirishaji holela wa korosho kwa njia mbalimbali, huku wafanyabiashara wakiendelea kubuni njia hizo ili kukwepa mkono wa sheria.

Hatua hiyo imesababisha hali ya kuwindana na huku wengine wakiwarubuni wakulima ili kuwauzia korosho kwa njia isiyo halali maarufu kama ‘kangomba’.

Utoroshaji huo umekuwa ukizigharimu halmashauri kutokana na kupoteza mapato mengi yatokanayo na zao hilo ili kupigana vita hiyo inayolenga kuharibu utaratibu uliowekwa na Serikali.

Katika maeneo mbalimbali mkoani Mtwara, wakulima wameonekana kulalamika baada ya Serikali ya mkoa kusimama imara katika usimamizi wa zao hilo, huku doria mbalimbali zikifanywa usiku na mchana na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wanaokiuka utaratibu.

Katika doria hiyo, Wilaya ya Newala imefanikiwa kukamata zaidi ya kilo 300, huku wakishikilia pikipiki tatu zilizotumika kusafiria korosho hizo, hatua ambayo imeonekana kuwaogopesha wasafarishaji wengi wa zao hilo ambao hivi sasa wanatembea usiku ili kuweza kutorosha korosho hizo.

Pamoja na kuwa wabunifu katika kupitisha korosho na kuzificha mithili ya bangi huku Serikali ikiwabaini na kuzifahamu njia wanazotumia ikiwamo kuweka korosho kwenye madumu ya maji na kuzisafirisha kwenye pikipiki, huku nyingine zikiwa kwenye magunia ili kukwepa mkono wa sheria.

Hatua hiyo ya kuwapigania wakulima imekuja baada ya kuonekana kushamiri kwa uuzwaji huo haramu ambao umekuwa ukiwapatia faida ndogo, huku wanaouza kwa mfumo wa stakabadhi mazao ghalani wakinufaika na malipo makubwa kwa kuwa walilipwa hadi 2,900 kwa msimu wa mwaka 2015.

Ili kunusuru janga hili, Serikali inapaswa kutumia njia za ziada ili kudhibiti uuzwaji holela wa korosho ambao umekuwa ukiingizia hasara Serikali kutokana na kutolipwa kwa tozo, huku ikikosesha takwimu halisi ya mavuno katika mkoa na halmashauri husika.

Ifike mahala wakulima wanufaike na wapewe elimu ili kuwaondoa katika mawazo mgando juu ya kuuza korosho zao kwa kutumia kangomba ambayo imekuwa ikiwanyonya na kuwapa mapato madogo.

Wakulima wengi wanaonekana kuitumia hiyo njia ya kangomba, huku wengine wakifanya biashara ya kubadilishana na wafanyabiashara ‘barter trade’ korosho kwa mchele ama unga ili waweze kupata chakula, hii inaonyesha wazi kuwa wakulima wengi wanauza korosho zao kwa njia ya kangomba.

Ili wafanyabiashara wawe huru na biashara hiyo ya korosho, Serikali ilegeze masharti kwa kutoa elimu itakayowafanya wafanyabiashara hao kuacha matumizi ya kangomba na badala yake watambue njia halali za kuuza korosho zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles