24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kessy amfuata Ngassa

kessy2NA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

BEKI wa timu ya Simba, Hassan Kessy, yupo mbioni kujiunga na moja ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, anakocheza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Ngassa.

Kessy amesimamishwa kucheza mechi tano na klabu yake ya Simba baada ya kumchezea rafu mbaya mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mpango huo wa Kessy kwenda kucheza soka nchini Afrika Kusini ni wa muda mrefu lakini alikuwa akisubiri amalize mkataba wake unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA Jumamosi imezipata, zinasema kuwa kwa muda mrefu meneja wa mchezaji huyo, Athuman Tippo, amekuwa katika mazungumzo na timu ya Free State Stars pamoja na Bidvest Wits aliyowahi  kufanya majaribio mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.

Inaelezwa kuwa kusimamishwa kwake na Simba ni kama wamemrahisishia njia ya kwenda nchini humo kukamilisha mipango yake hiyo na muda wowote kuanzia sasa ataondoka.

“Tippo amekuwa na mipango ya kumpeleka Kessy kwenda kucheza soka la kulipwa kwa muda mrefu na tayari mazungumzo baina yake na timu za Free State na ya Bidvest yanaendelea, hivyo upo uwezekano mkubwa  Kessy asicheze Ligi ya Tanzania  msimu ujao iwapo mipango itakwenda sawa na kwenda kujiunga katika timu moja kati ya hizo,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Kessy kuzungumzia suala hilo, alikiri kuwa na mipango ya kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini ingawa hakuweka wazi timu anayofanya nayo mazungumzo hadi sasa.

“Ligi ya Tanzania inakwisha na mkataba wangu pia unamalizika hivyo ni wakati wa kuchagua mahali pa kwenda kucheza soka ambapo nitaona naweza kufanya kazi kwa uhuru, lakini ni mapema kusema timu gani naenda kikubwa ifahamike nitakwenda kucheza soka Afrika Kusini,” alisema Kessy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles