Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
Kesi za Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo ambaye anadaiwa kupotea, zimesikilizwa katika mbili tofauti jijini Dar es Salaam na Iringa.
Wakati Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, ikiutaka upande wa serikali kujibu maombi ya mawakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Mtandao wa Wanafunzi (TSNP) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ifikapo Machi 26 mwaka huu katika kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP).
Wakati huo huo, Nondo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa na kusomewa makosa mawili ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni na kudanganya kutekwa.
Wiki iliyopita, mawakili THRDC, TSNP na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu waliwasilisha maombi Mahakama Kuu kuitaka itoe amri kwa Jeshi la Polisi kumpeleka Nondo mahakamani au kumpa dhamana wakati shauri la msingi likiwa linaendelea.
Wakili wa Nondo, Paul Mpoki amedai kuwa maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na kuitaka mahakamani hiyo kumpa dhamana mteja wake, kumpeleka mahakamani ama kumuachia huru.
Akisoma uamuzi mdogo leo Jumatano Machi 21, Jaji wa mahakama hiyo Rehema Sameji amesema upande wa waleta maombi utajibu hoja hizo Machi 27 na mahakama hiyo utaanza kusikiliza kesi hiyo Aprili 4, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Nondo anatetewa na mawakili sita wakiongozwa na Mpoki na Jebra Kambole huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili ambao ni Keneth Sekwao na Beatha Mtau.