Kesi ya ufisadi inayomkabili Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma (75), imeahirishwa hadi Juni 8 mwaka huu.
Kesi hiyo ambayo mashtaka yake yanatokana na mpango wa Afrika Kusini kununua silaha mwaka 1990, ilisikilizwa mapema leo katika Mahakama Kuu mjini Durban ambapo Zuma alifika kortini ili kusikiliza mashtaka dhidi yake.
Zuma ambaye alilazimishwa kujiuzulu mwaka huu, anakabiliwa na mashtaka 16 yanayotokana ulaghai, utapeli, rushwa pamoja na utakatishaji wa fedha.
Kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani ilitupiliwa mbali mwaka 2009 lakini Mahakama Kuu ya mjini Pretoria iliwahi kusema kuwa, uamuzi uliotolewa mwaka 2009 haukuwa na mantiki na kwa msingi huo, kesi hizo zinafaa kusikilizwa upya.
Awali, baadhi ya wanachama waandamizi wa ANC walimtaka Zuma kuachia ngazi, wakitumia hoja ya madoa yaliotiwa kwa chama hicho na kashfa kadhaa za rushwa, kufuatia matokeo mabaya kabisa ya uchaguzi wa manispaa uliofanyika Agosti 2016.
Hata hivyo, malumbano kati ya Zuma na chama cha ANC yalipelekea kuondolewa kwake kama kiongozi wa chama hicho na nafasi yake kuchukuliwa na makamu wake wa rais, Ceril Ramaphosa mwezi Desemba mwaka wa 2017.
Zuma ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka wa 2009, kufuatia kujiuzulu kwa Rais Thabo Mbeki, ambaye pia alikabiliwa na tuhuma mbali mbali.