31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

BASHE ATAKA SERIKALI IUNDE CHOMBO KUCHUNGUZA MAUAJI YA MUUZA MACHUNGWA MBEYA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuunda chombo maalumu kuchunguza mauaji ya muuza machungwa Allen Mapunda (20), anayedaiwa kuuawa mkoani Mbeya kwa kupigwa na polisi.

Akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni leo Ijumaa aprili 6, Bashe amesema chombo hicho kitaondoa utata uliopo sasa ambapo wazazi wa marehemu wadai mtoto wao alipigwa na polisi huku jeshi hilo likikanusha kuhusika.

“Yapo mambo ambayo yanaanza kutokea ambayo yanaashiria kuanza kuwepo kwa migawanyiko katika taifa letu na mambo haya tukiendelea kuyatizama kwa macho, hayaleti taswira njema huko mbele na wala hayataweza kulifanya taifa hili kuwa moja wala kupambana na adui mkubwa ambaye ni umaskini.

“Yanatokea matukio ya kusikitisha katika nchi yetu, ambayo ukitazama huoni chombo chochote kikichukua jitihada za makusudi ambayo itawajengea Watanzania imani kwamba hata mimi mdogo nikiwa mkubwa yupo anayenilinda.

“Yamekuwa yakitokea matukio mengi na kukosa majibu katika nchi yetu, lipo tukio la kijana anaitwa Allan ambaye ni muuza machungwa pale Mbeya.

“Naiomba serikali kwa heshima kabisa, matukio ya namna hii yakiendelea kujengeka katika nchi yetu yataanzisha utamaduni wa kutowajibika, yanaharibu amani iliyo katika taifa letu.

“Kijana huyu amefariki, ripoti ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, inasema kijana huyu kafariki kwa majeraha ya ndani ya mwili wake.

“Familia yake inasema waliompiga ni jeshi la polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya anasema hawahusiki, matokeo yake serikali imeenda kutoa rambirambi ya Sh 200,000,” amesema Bashe.

“Hii ndiyo sababu matukio ya namna hiyo yameendelea kuwepo, mimi ningeiomba Wizara ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu, waagize kuundwa kwa chombo rasmi huru ifanye uchunguzi ya haya mambo.

“Hatuwezi kuacha hii hali ya utamaduni wa kutojali ikaendelea katika nchi yetu, inahuzunisha na inaharibu taswira na hii ndiyo inatumika na watu wasiopenda nchi yetu kuendelea kuharibu heshima ya taifa letu. Naiomba serikali ichukue hatua katika jambo hili, hili ni jambo la msingi sana,” amesema Bashe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles