
NA JUDITH NYANGE, MWANZA
SHAURI la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kuiomba Mahakama kubatilisha amri polisi kuuzia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa limepangwa kuanzwa kusikilizwa leo.
Tofauti na yalivyokuwa maombi yaliyowasilishwa Juni 10, mwaka huu katika shauri la namba 79 la mwaka 2016, mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza yaliyowajumuisha washtakiwa watano, shauri la sasa litajumuisha washtakiwa wawili ambao ni Kamanda wa Polisi Wilaya ya Geita (OCD) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Shauri la awali namba 79 la mwaka 2016 liliwajumuisha washtakiwa watano wakiwamo Kamanda wa Polisi Wilaya ya Geita na Kahama, Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Juni 14, mwaka huu, Jaji Mohamed Gwae, alibaini upungufu wa sheria katika shauri hilo kwa kumjumuisha Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Nsato Mssanzya ambaye kisheria anastahili kufunguliwa mashtaka masijala kuu.
Jaji Gwae aliwasahauri mawakili wa Chadema kurekebisha hati yao.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza jana, Mbowe alisema shauri hilo litaanza kusikilizwa kesho (leo) mbele ya Jaji Gwae.
Katika shauri hilo, Mbowe kupitia kwa Mawakili wake, Paul Kipeja na John Malya amewasilisha maombi manne yanayohusu kutafuta haki ya kufanya mikutano na mikusanyiko ya siasa iliyozuiliwa na polisi Juni 7, kupitia kwa Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi Makao Makuu, Nsato Mssanzya.
Mbowe ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kutamka kuwa amri iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Geita (OCD) kuzuia mikutano ya hadhara iliyopaswa kufanyika Katoro na mjini Geita kuwa si sahihi na ni kinyume cha sheria.
“Ombi jingine tumeiomba mahakama kutengua amri ya OCD wa Geita aliyoitoa Juni 7, 2016 kuzuia mikutano ya hadhara ya Chadema iliyokuwa imetangazwa na kupangwa kufanyika wilayani humo kuanzia tarehe hiyo, kwa muda usiojulikana.