24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mgeja: Mkapa afikishwe mahakamani

Khamis Mgeja
Khamis Mgeja

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Taasisi ya Tanzania na Maendeleo, Khamis Mgeja, amesema Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, anapaswa kuwa mtuhumiwa wa kwanza kupandishwa kizimbani katika mahakama ya mafisadi inayotarajiwa kuanzishwa Julai mwaka huu.

Amesema kiongozi huyo ndiye alihusika na kuisababishia hasara Serikali ikiwamo kuota   mizizi ya ufisadi serikalini.

Mgeja  amesema  pia kuwa Rais Dk. John Magufuli, anapaswa kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya haraka katika baadhi ya sheria zinazowalinda viongozi kama njia ya kuondoa mfumo unaokumbatia wahalifu.

Hayo aliyasema   Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema  Rais  Magufuli akiamua kutenda haki katika kuwawajibisha mafisadi na wahujumu uchumi  anapaswa kuanza na Rais Mkapa.

“Juzi,  Mkapa tumemsikia kwenye mdahalo anaomba radhi, angekuwa muungwana  angeenda mahakamani kwa makosa aliyowatendea watanzania, tunamuomba rais Magufuli  aanze kumshughulikia Mkapa  kupitia mahakama ya mafisadi na wahujumu uchumi   aimbie dunia makosa aliyoyafanya.

“Mkapa ni jipu ila limekaa pabaya ikiwezekana rais asaidiwe,” alisema Mgeja.

Mgeja   alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka  2015.

Alisema Rais mstaafu Mkapa ndiyo chanzo cha nchi kuwa maskini kwa kuwa  aliuza rasilimali kwa bei ya kutupwa   na kuruhusu ubinafsishwaji  holela nchini.

“Utetezi anaoendelea kuutoa kwa wananchi majukwaani baada ya kutoka madarakani  haujitoshelezi kwa kuwa  makosa aliyoyafanya ni mazito, angekuwa muungwana angeenda mahakamani kutuomba radhi,” alisema Mgeja.

Alisema  taasisi hiyo haimani kama Mkapa alifanya mambo hayo kwa bahati mbaya  kwa kuwa alikuwa akitoa uamuzi kupitia Ikulu ambayo ni taasisi yenye wataalamu ambao wangeweza kumshauri vizuri au hata kumzuia.

“NBC kaiuza kwa Sh bilioni 16 wakati ilikuwa na mali ya zaidi ya Sh bilioni 100 …  wakati anatoa uamuzi  huo alikuwa mzima au alikuwa amejitwanga (kulewa) kwa sababu ni mwanachama mzuri wa hiyo kitu,” alisema Mgeja.

Akizungumzia uamuzi wa aliyekuwa mmoja wa wanachama wa Chadema, Goodluck ole Medeye kuhamia UDP,  alisema   mpaka sasa anaona Chadema ndiyo chama pekee cha upinzani ambacho kina nguvu  ya kuondoa CCM katika dola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles