Na UPENDO MOSHA -MOSHI
UPANDE wa Jamuhuri katika kesi ya msingi ya mauaji ya mfanyabishara, bilionea Erasto Msuya umekata rufaa juu ya uamuzi wa mahakama wa kukataa ushahidi wa maelezo yaliyotolewa kwa mdomo na shahidi wa tisa.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama dhidi ya shahidi namba tisa, Inspekta, Samuel Maimu, ambako upande wa Jamhuri haukuridhika na uamuzi wa Mahakama uliotolewa awali.
Mahakama ilitoa uamuzi wa kukataa ushahidi uliowasilishwa kwa njia ya mdomo mara mbili na shahidi huyo, baada ya mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Wakili Majura Magafu, kuwasilisha pingamizi la kukataa ushahidi huo kwa vile ni kinyume cha sheria.
Wakiwasilisha hati ya kuomba kukata rufaa, mawakili wa upande wa Jamuhuri wakiongozwa na Wakili Omari Kibwana, walisema wameamua kupeleka hati ya kukata rufaa dhidi ya ushahidi uliowasilishwa kwa njia ya mdomo.
Kabla ya kuibuka malumbano ya sheria baina ya mawakili wa upande wa utetezi na Jamhuri, shahidi huyo akiongozwa na wakili wa upande wa Jamhuri, Abdala Chavula, alidai kuwa Agosti 13 mwaka 2013 mtuhumiwa namba tano alikiri kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Sehemu ya mahojiano ilikuwa hivi:
Wakili: Shahidi, ebu ieleze mahakama hii Agosti 13 mwaka 2013 wakati ukizungumza na mtuhumiwa alikueleza nini?
Shahidi: Alieleza kuwa yeye ndiye aliyekuwa amekamata bunduki na kumuua Erasto Msuya.
Wakili: Je siku iliyofuata baada ya kumuhoji mtuhumiwa nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya kumkamata tulifunga safari siku inayofuata kuja Kilimanjaro.
Wakili: Nini kilijiri ulipofika Kilimanjaro?
Shahidi: Tulimpeleka kwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro wakati huo alikuwa ni Ramadhani Nganzi na pia mtuhumiwa alikiri kweli kuhusika na mauaji ya Msuya.
Wakili: Maneno hayo aliyasema wapi na nani ulikuwa naye.
Shahidi: Aliyasema maneno hayo kwa RCO na mimi pia nilikuwapo nikisikia akiongea na pia tulikuwa na askari, Koplo Atwai ambaye tulikuwa naye safarini kurudi Kilimanjaro.
Wakili:Baada ya kueleza nini kilifuata?
Shahidi : Afande RCO alitoa maagizo kwamba tumpeleke kwa mlinzi wa amani na baadaye aliwekwa mahabusu kwa ulinzi.
Wakili: Jana ulisema kule mlikuwa na watuhumiwa wawili. Je mwingine mlimuacha wapi mkiwa kule Tabora ?
Shahidi: Mtuhumiwa mwingine ambaye ni Sadiki alikuwa kwenye gari.
Wakili: Eneo mlilokuwa wakati huo ni eneo gani
Shahidi: Kijiji cha Rimbura
Wakili: Na baadaye mlimpeleka wapi?
Shahidi: Tulimpeleka mpaka Kituo cha Polisi Kaliuwo.
Wakili: Baada ya kufika kituo cha polisi Kaliuwo nini kiliendelea kwa Sadiki?
Shahidi : Aliwekwa mahabusu mpaka kesho yake
Wakili: Nini kilitokea?
Shahidi:Alisema anataka kwenda Limbula kuna vitu aliviacha, tulienda lakini sikuona fedha na baada ya kutoka Lembula na kufanya upekeuzi hatukuona kitu chochote. Tulirudi nayee tena kituoni na baada ya kufika waliandika tena maelezo yao.
Wakili: Shahidi ebu eleza uhusika wa mtuhumiwa namba sita ulikuwa vipi?
Shahdi: Alisema siku ya tukio alikuwa na pikipiki moja na walikuwa maeneo ya Mjohoroni Bomang’ombe na walikuwa wakiangalia kama kuna dharura waweze kumsaidia Karimu na baada ya mauaji waliondoka na pikipiki.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Magafu ulisema: “Tunashikitishwa kuona upande wa mashtaka wanatumia sheria vibaya kwa kuwaadhibu watuhumiwa kuendelea kukaa ndani kwa sababu kila hatua tunayopiga wao wanakimbilia kukata rufaa ili tu kesi isimame. Ni kweli kukata rufaa ni haki yao kisheria lakini ni kwa sababu tu za msingi sisi hatujafurahishwa na jambo hilo.
Kesi hiyo ya mauji ya Mfanyabiashara wa Madini, Erasto Msuya yaliyotokea Julai 7 mwaka 2013, itaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.