Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ametoa wito kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha wanatanua wigo wa usambazaji wa gesi asilia kwa kushirikiana na sekta binafsi. Lengo ni kuhakikisha gesi asilia inawafikia Watanzania wengi zaidi kwa haraka.
Mramba ametoa kauli hiyo Jumanne, Julai 9, 2024, alipokuwa akitembelea banda la TPDC katika maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba.
“Tunataka gesi inayopatikana nchini isambae kwa haraka zaidi na kuwafikia Watanzania. Gesi ifike katika vituo vya kujazia magari na majumbani. Changamoto yangu ni kuona ni kwa namna gani sekta binafsi inaweza kushirikishwa katika usambazaji wa gesi. Ikiwa tutamtegemea TPDC pekee kwa kasi yake, itachukua muda mrefu kuwafikia Watanzania wote,” alisema Mramba.
“Lakini tukishirikisha sekta binafsi, wakaweza kusambaza mabomba na gesi ya majumbani, pamoja na vituo vya kujazia nchi nzima, basi gesi tuliyonayo itasambaa kwa haraka,” aliongeza.
Mramba alieleza kuwa TPDC inasimamia utafutaji, uchimbaji, na usambazaji wa gesi asilia sambamba na utafutaji wa mafuta, ikiwamo mradi mkubwa wa bomba la mafuta la EACOP. Alisema TPDC imekuwa ikifanya kazi kubwa na nzuri, lakini bado kuna nafasi ya kuboresha zaidi.
“Kwa mfano, hapa ndani nilikuwa naongea na kampuni tanzu ya TPDC, GASCO, ambayo kwa muda mrefu imepata uzoefu katika kujenga na kusimamia miundombinu ya gesi. Wamejenga mabomba kadhaa ya gesi maeneo ya Mtwara, Dar es Salaam ikiwamo Sinza, Kijitonyama, na Mbezi Beach. Wito wangu kwa GASCO ni kujitangaza zaidi, kuna Watanzania wanahitaji huduma zao lakini hawajawahi kujitangaza,” alisema Mramba.
Katibu Mkuu alieleza kuwa nia ya Serikali ni kuona TPDC inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. Alisisitiza kuwa maonyesho kama Sabasaba ni fursa kwa wananchi wa kawaida kupata uelewa juu ya shughuli zinazofanywa na taasisi za umma.
“Kwa mfano, GASCO wanajenga vituo vya mafuta, lakini ni watu wangapi wanafahamu? Wapo wafanyabiashara wanajenga vituo vya mafuta na wakati mwingine hawajui mkandarasi wa kuwajengea kituo hicho watampata wapi. Lakini kumbe tuna taasisi yetu ya GASCO yenye wajuzi na wataalamu wa kufanya hivyo,” alieleza Mramba.
Aliongeza kuwa GASCO pia inajenga vituo vya CNG vya kusambaza gesi na kuweka gesi kwenye magari, lakini watu wengi hawajui kama wanatoa huduma hiyo. “Mtu anayemiliki kituo cha mafuta angependa kuongeza huduma ya kujaza gesi kwenye magari, ni GASCO wenye uwezo wa kutoa huduma hiyo,” alisema.
Mramba alihitimisha kwa kusema kuwa hadi kufikia mwaka 2025, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itakuwa imekamilisha ujenzi wa zaidi ya vituo 30 vya kujazia gesi asilia jijini Dar es Salaam.