Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imeanza kusambaza nakala milioni mbili za Katiba inayopendekezwa nchini kote ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya nakala hizo zilizochapwa, 1,800,000 zinasambazwa Tanzania Bara na 200,000 upande wa Zanzibar.
Dk. Migiro alisema hadi kufikia juzi, jumla ya nakala 707,140 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo imepata 200,000 na kwamba kazi hiyo inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi ujao.
Aliitaja mikoa ambayo imesambaziwa nakala hizo ni Katavi (15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540), Kigoma (41,440), Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambako usambazaji umeanza kwa Wilaya ya Mafia iliyopata nakala 2,400.
“Idadi ya nakala za Katiba inayopendekezwa kwa kila mkoa inategemea na wingi wa kata katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona imepata nakala nyingi,” alisema Dk. Migiro.
Kwa mujibu wa Waziri Migiro, kuna zaidi ya kata 3,800 nchini kote na lengo la Serikali ni kusambaza nakala 300 kila kata, ambazo zitasambazwa kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji.
Pamoja na usambazaji huo, Waziri Migiro aliwakumbusha wananchi ambao bado hawajapata nakala za Katiba inayopendekezwa, kuisoma kupitia tovuti ya Wizara ya Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz) na tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz).