29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa nzito vituo vya afya, hospitali

Waziri akiri mchezo wa kubambikia watu magonjwa, aonya hakuna kipimo cha UTI, homa ya matumbo kinachotolewa chini ya saa mbili  hadi 72

NA AGATHA CHARLES, DAR ES SALAAM

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto imekiri baadhi ya vituo vya afya na hospitali za sekta binafsi kuwa na mchezo wa  kuwabambikia watu wagonjwa kwa nia ya kufanya biashara.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile alipotafutwa na MTANZANIA Jumapili lililotaka kufahamu sababu za baadhi ya vituo vya afya hususani vile binafsi kutoa  majibu ya vipimo vya magonjwa yanayotofautiana kwa siku moja na kwa mtu mmoja.

Dk. Ndugulile alisema jambo hilo hufanywa kutokana na ukosefu wa weledi na maadili ya kazi hiyo ya utoaji huduma kwa binadamu.

“Baadhi ya vituo vya afya vya sekta binafsi wameamua kufanya biashara katika magonjwa ya watu. Wamekuwa wanawabambika magonjwa ambayo wagonjwa hawana kwa lengo la kujinufaisha na sisi tunaendelea kutoa elimu kwa jamii,” alisema Dk. Ndugulile.

Alitoa mfano vipimo vya ugonjwa wa maambukizi katika mfumo wa mkojo (UTI)  na  homa ya matumbo (typhoid) kuwa kwa taratibu za kitabibu ili kupata majibu huchukua  si chini ya saa mbili hadi 72.

Alipoulizwa wao kama Wizara ya Afya wapo tayari kufanya uchunguzi juu ya jambo hilo, Dk. Ndugulile alisema;

“Mtu dakika 15 anasema una UTI, mara nyingi wagonjwa wanapata matibabu ambayo si sahihi. Tunatoa elimu kwa umma, ni ngumu kuchukua hatua bila kuletewa malalamiko, tukipata taarifa tunachukua hatua,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema asilimia 70 ya homa si maralia, UTI wala ‘Typhoid’ bali mara nyingi  huwa ni virusi ambavyo vinapita.

Kutokana na hayo Dk. Ndugulile alisisitiza kuwa mara kadhaa amekuwa akiwataka watoa huduma kuzingatia weledi na maadili.

Juzi, gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi, katika ukurasa wa maoni yaliandikwa maoni ya gazeti yakiitaka Wizara ya afya ichunguze sintofahamu ya kutofautiana vipimo  kutoka kituo na hospitali moja hadi nyingine kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya watu wengi.

Ndani ya tahariri hiyo, Mhariri alieleza kuwa Wizara hiyo inapaswa kufuatilia vipimo na aina ya matibabu yanayotolewa katika vituo vya afya na hospitali zote nchini.

Maoni hayo yalitokana na malalamiko kadhaa kutoka kwa jamii ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwa baadhi ya watu wanaofika kupata huduma ya afya ikiwamo mtu kupimwa katika kituo kimoja au hospitali moja kisha kuambiwa ana maralia, UTI, homa ya matumbo lakini mtu yule yule akienda katika kituo kingine majibu huwa ni tofauti.

Mfano unaothibitisha hilo ni wa Atu Chrispin ambaye hivi karibuni baada ya kupata homa kali alifika katika kituo kimoja kilichoko Temeke, Dar es Salaam na baada ya kupima Malaria, UTI, Typhoid aliambiwa hana lakini alipokwenda kituo kingine cha afya aliambiwa ana malaria na Typhoid.

Yeye mwenyewe anasema; alipokwenda kituo cha kwanza na vipimo kuonyesha hana tatizo lolote, Daktari aliyemuhudumia alishauri apimwe ugonjwa wa Dengue ambao ulionekana lakini alipolazwa na kupata  matibabu hali iliendelea kuwa mbaya hata baada ya kuruhusiwa.

“Watoto wangu waliamua kunipeleka hospitali nyingine ambayo huko baada ya kupimwa niliambiwa nina Malaria mbili na ‘Typhoid’, vipimo vilitoka baada ya saa moja na nilipoanza kutumia dawa nilizoandikiwa nilipata nafuu na baadae nilipona kabisa” alisema.

David Kambimtoni anasema kuna wakati alisikia homa na alipoamua kwenda kituo kimoja cha Afya jijini Dar es Salaam  baada ya kupima malaria na typhoid majibu yalionyesha ana tatizo.

“Niliandikiwa dawa lakini sikunywa nikasema hapana lazima nijiridhishe, nikaamua kwenda hospitali nyingine nikapima vipimo vilevile lakini nikawadanganya kwamba nimetumia dawa siku nane zilizopita lakini bado najisikia vibaya,  yule mtu wa maabara aliniambia kama nimetoka kutumia dawa mara nyingi ugonjwa si rahisi kuonekana na kweli majibu yalipotoka ikaonekana sina malaria wala typhoid.

“Sikuridhika nikaenda hospitali nyingine ya tatu nikapima vipimo vile vile, safari hii sikuwaambia chochote majibu yalipotoka nikaonyesha sina chochote, imepita miezi mingi sasa zile dawa sikunywa na ninajisikia vizuri kabisa, kwahiyo ni jambo ambalo kidogo linaleta ukakasi kwa vipimo kutofautiana, unajiuliza maswali mengi,” alisema.

Tukio hilo linawapata wengi na wapo watu ambao wanahisi kwamba huenda nyakati fulani walipata matibabu ambayo si sahihi kutokana na vipimo vya hospitali moja hadi nyingine kutofautiana.

Hali  ambayo wengi wanasema kwa kiasi kikubwa in imewaacha katika sintofahamu na hata wakati mwingine kupoteza imani na aina ya matibabu wanayopatiwa katika hospitali au vituo vya afya.

Zaidi  wengi wamekuwa wakihoji uhakika na ubora wa vifaa vinavyotumika katika vituo na hospitali mbalimbali.

Wengine wamekwenda mbali na hata kuhoji utalaamu wa wale wanaosoma majibu ya vipimo maabara kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo.

Pengine kutokana na sintofahamu hiyo wapo walioshauri kwamba pengine ni wakati muafaka kwa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufuatilia kwa kina jambo hilo ili kunusuru watanzania wanaopatiwa matibabu ndivyo sivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles