Na Shermarx Ngahemera na Mitandao
MGOGORO wa kibiashara wa kujitakia kati ya Marekani na China katika mtindo wa nani zaidi, umefikia hatua mbaya na hivyo kutegemewa kuharibu biashara ya kimataifa kwani msingi wake ni ubabe wa Kimarekani na mfumo kinzani wa uchumi wa China (modeli spesheli ya China) na ujanja wa kibiashara wa China unaotetea masilahi yake zaidi.
Mfumo huo wa China unaofaidisha nchi yake haujazoeleka machoni kwa wengi hasa nchi za magharibi zinazoongozwa na Marekani.
Wakati Marekani ina sera ya uhafidhina ya kiuchumi, China ina sera ya ubepari wa kitaifa (state capitalism) inayochanganya miliki ya kiserikali katika uchumi na ushiriki wa sekta binafsi katika maeneo lengwa kimkakati.
Mitazamo hiyo miwili imekuwa inasuguana kwa madai kuwa ushiriki wa Serikali ya China unasababisha uwepo wa hali isiyo tambarare kiuchumi na hivyo kuiongezea China uwezo mkubwa kiushindani kibei, kwani mwisho wa ushiriki wa Serikali katika uzalishaji wa bidhaa hizo unashindwa kujulikana kikomo chake.
Hali hiyo inaonekana kumpa taabu Rais Trump ambaye anataka iondolewe ili bidhaa zishindane bila hofu wala mwingiliano na upendeleo; China imekataa na hivyo kuanza kuwekewa vikwazo bidhaa zake ziwe ghali na zisinunuliwe.
Historia inaonesha miundombinu yote ya biashara na kiuchumi duniani imeundwa ili kunufaisha nchi ya Marekani na marafiki zake katika kundi la G7 ambako China hayumo ingawa hualikwa kushiriki na kundi hilo lilimwingiza Urusi kwa hila na kuwa G8 ili kuteka rasilimali zake za gesi na mafuta, lakini Urusi imesimama kidete na kukataa kutoa vitu kwa dezo na sasa wanaipelemba nchi hiyo kwa kuiwekea vikwazo ili isalimu amri lakini imedinda.
Hasimu mwingine wa uchumi kwa nchi za Magharibi ni Iran ambayo inautajiri mkubwa wa mafuta ambao ungenufaisha nchi za Ulaya. Awali Iran ilifanya hivyo lakini Ayatollah Khomeini alibadilisha kwa Mapinduzi ya mwaka 1978 ambapo kibaraka Mfalme Shah Reza alipoangushwa na kukimbilia Ufaransa na Khomeini kutoka Ufaransa na kurudi Tehran kutawala nchi kama Dola ya Kiislamu na hivyo kuiweka pagumu Marekani na uchumi wa mafuta ya dezo na kufanya utawala huo kuwa adui mkubwa wa Marekani.
Mazungumzo na mkataba wa Nyuklia ya Iran na mataifa makubwa 6 ikiwamo Marekani, Uingereza, Ufaransa, China , Urusi na Ujerumani ambayo yalizima mvutano wa amani duniani alipoingia Trump yakawa lengo lisilo jema na kuvurugwa na Trump pekee kuwa halifai na kujitoa kwani anadai lilimpa sana madaraka Iran badala ya nchi hizo kumlazimisha asalimu amri.
Hii ilifanywa na Trump ili aweze kuwafurahisha marafiki zake wenye kampuni za silaha ambao huishi kwa damu za vita na ulazimu wa kununua silaha kutoka Marekani kwa kujihami kwa vita fikirika. Ni biashara ya nchi kubwa kijeshi ikipigiwa chapuo na Israel kule Mashariki ya Kati!
Dola la Marekani kwa miaka mingi limekuwa na mazoea na kufikia kiwango cha kuwa ni utamaduni wa kuburuza nchi nyingine zifuate matakwa yake ima faima lakini safari hii China imesimama kidete kupambana.
Inataka kupambana na dubu anayetaka kumaliza upinzani wowote dhidi ya utawala wa Marekani ambao unataka kuona China inasalimu amri kwa kutekeleza matakwa ya Rais Donald Tump ambaye ujaji wake umeifanya dunia iendeshwe kivingine. Sasa duniani mambo ni juu chini ili kurudisha kwa nguvu uongozi wa Marekani katika medani zote ikiwemo za vita kwenye kile kinachoitwa Dola ya Marekani (American Empire ) ambayo ipo tokea mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na Vita Baridi.
Kiuchumi sasa Marekani inaongoza duniani ikifuatiwa na China ambayo ilichupa kutoka uchumi namba sita hadi kuwa namba mbili duniani bila kwenda hatua kwaa hatua kama zilivyofanya nchi nyingine wakati wa kupanda.
China inaona inaweza kiushindani na kutokana na nguvu hiyo na aina ya uchumi wake thabiti imeifanya Marekani kuingiwa hofu ya kunyang’anywa nafasi adhimu ya kuwa namba moja ambapo Washington ikitamka ulimwengu wote unatekeleza! Sasa thubutu!
Lakini kila kitu kikali kina ncha nayo makali yana mwisho wake ; inaonekana wakati umefika wa Marekani kushuka ngazi polepole lakini kwa uhakika. Ni kweli ngumu kumeza na haswa kwa Trump ambayo uzoefu wake mambo ya serikali ni biashara zake!
Lakini China inayo uwezo ila nia haina kwa kuogopa majukumu yatokanayo na nafasi hiyo ya ubeberu kwani yenyewe inasema kuwa inauchumi mkubwa lakini haijaendelea sana na hivyo kutaka kujiimarisha kwanza kwa kuendeleza watu wake badala ya ushindani wa kivita usio na faida bali utapanyaji mali na kutoa machungu kwa wengi.
Uchumi wake China ni uchumi dola wa kupanga kufuatana na mahitaji ya nchi hiyo wakati Marekani ni uchumi holela wa watu binafsi au Mashirika makubwa (corporations) unaofuata mahitaji ya soko na hivyo chumi hizo zinakinzana na kuona mwinzie anacheza faulo kwani uwanja unadaiwa kuwa sio tambarare.
Viashiria vingi vinaonesha kiukweli yenyewe ndio namba moja (de facto) kwani Marekani ni mdaiwa wake mkubwa kwa kiasi cha zaidi ya Dola Trilioni 18 na hata miji mingi ni mali ya China kwani inahodhi hisa zake (state bonds) kwa hiyo ni kazi moja tu ya China kuita madeni hayo na Amerika kuwa chini kama haitajali na kuchukua silaha zake za nyuklia na kukataa. Wajuzi wanasema hiyo sio rahisi hadi kwa mnyukano!
Lakini kufanya hivyo ni kuuweka rehani ulimwengu mzima kibiashara na kiuchumi na hivyo imeamua kucheza shere na Marekani ili mambo yake yasonge mbele kwanza na kuachia ngazi bila aibu kubwa kama anavyotaka Trump kufanya wakati huu kwa kuiadhirisha China ingawa haina kosa la wazi ila ni ubeberu tu.
Kadiri siku zinavyokwenda mkakati huo wa China unaonekana ni mgumu kwake kwani Trump anataka kupunguza deni hilo kwa kubadirisha mwenendo wa biashara kwa kuongeza tozo kwenyte bidhaa za China na hivyo mwishowe deni litapungua au kuilazimisha China ipunguze thamani ya fedha zake ili aweze kuuza Marekani; masuala yote mawiliChina imeyakataa kwani hakuna haja na hayahitaji na kumfanya Trump awe mbogo.
Trump anaongeza idadi bidhaa na thamani ya tozo hadi dola bilioni 250 na kufanya mambo yawe magumu China kwani ilijibu mapigo hayo kwa tozo duni na dhaifu kwa thamani na kuonekana Marekani imeshinda kinadharia lakini kiukweli ngoma bado mbichi kwani China hailazimiki kuuza bidhaa zake Marekani ingawa ndiye mnunuzi mkubwa. Isitoshe inao watu wake wengi duniani na hivyo ikishindikana China itauza bidhaa zake nyumbani au kwa mfumo mwingine au kupitia nchi nyingine ili deni la Marekani lisiendelee kukua na kumwingizia ufukara wake.
Isichoelewa Marekani mbele ya Jumuia ya Kimataifa yenyewe ndio mhalifu yaani anakopa hataki kulipa na akitaka kulipa afanye hivyo kwa mashariti yake kwa mbinu ya kuongeza tozo ili ifute deni yaani anamkata China mapato yake halali kwa dai kuwa ni kodi.
Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa kuwa kinachofanyika na baadhi ya nchi kwa nchi yake kuwekewa vikwazo ni “uharamia wa kiuchumi” na hivyo kutishia usalama wa Dunia kwani unafanyika bila uwajibikaji kwa misingi ya kimataifa na vigezo vya mwenendo wa taasisi za kimataifa.
Akasema kupuuza maoni ya mataifa mengi sio uhodari na ukuu bali ni ishara ya mapungufu ya kutumia akili katika kuelewa uwepo wa mifumo mchangamano ya kimataifa inayowiana na kuingiliana kwenye dunia. Alisema ameridhika na jumuia ya kimataifa iliyosimama kidete kupinga kutengwa nchi yake na kulaani kauli ya Rais Trump kuwa anafanya juhudi ya kutaka kumpindua na kuangusha utawala wake Rouhani. Hizi ni siasa za kibeberu.
Kwa namna yake Uturuki nayo inatishiwa na Trump kuwa itatiwa adabu na imewekewa vikwazo. Ankara imekataa tishio na vikwazo hivi na kudai kuwa itaheshimu misimamo yake rasmi na Trump ni wa kupita tu na kujipa moyo kuwa sera hizo sio za Marekani bali ni za Trump binafsi ambaye anaonekana kutojua namna uhusiano wa kimataifa unavyoendeshwa na kudai kwenye uwazi vile vinavyoshugulikiwa kwenye faragha na hivyo havikubaliki. Nchi lazima ziheshimiane sio kwamali bali kwa asili(sovereignity).
Fimbo kubwa anayotumia Trump ni fedha yake ya Dola ambayo imeacha kutoka kuwa fedha ya mabadilishano katika biashara na yenyewe sasa kuwa ni bidhaa na kuanzisha maduka duniani kote ya kuuza na kununua fedha hiyo na kama rasilimali za nchi.
Dunia inahitaji mabadiliko ya kiuchumi ambao unatakiwa utenganishwe na mahitaji rasmi ya Marekani bali uwe shirikishi na kuchukulia mahitaji mapana ya dunia kama kijiji kikubwa kinachotegemeana na sio kuburuzana.
Kuingilia siasa Marekani
Marekani imeanza kutoa kauli tata kuwa China inaingilia uhuru wa Marekani kwa kutaka kuwe na mabadiliko nchini humo ambayo yatazuia uimara wa Trump na chama chake cha Republican kushindwa kwenye uchaguzi unaokuja wa muhula wa kati na Serikali za mitaa na majimbo.
Awali serikali ya Marekani ilidai Urusi imeingilia kati uchaguzi uliomwingiza Trump kwenye madaraka hali ambayo ilihamanisha wadau wa demokrasia duniani kote kwani wanaona kuwa sasa Marekani inaanza kukosa mwelekeo na kujiamini ambayo ni hulka mbaya kwa nchi kubwa kama hiyo kwani inaweza kuanza kutenda yasiyo stahili na inakatisha tamaa nchi nyingi ambazo zinachukulia kuwa ndio taifa la kuigwa kwenye Demokrasia . Hizo lawama zinashusha hadhi ya nchi hiyo na sio kuipaisha kama yenyewe ilivyotaka.
Watu wengi wanataka Trump akubali kusikia maneno ya wengine na kukosolewa kwani Marekani kwa dhana ya Dola ya Marekani ni kubwa sana kuingizwa kwenye mchakato wa kura kwani sio stahiki yake.
Sauti za vita
Shirika la habari la Uingereza, Reuters linasema kuwa ukinzani wa dhana na maana kati ya China na Marekani umefikia kubaya kwa nchi hizo kuanza kupigana vijembe na maneno ya vijimambo yaliyojaa uhasama na tambo.
Kutoka Tianjin, wiki iliyopita China imesema haitajiinamisha kwa thamani ya ushindani wa fedha zake, kwa kupunguza kiwango chake alisema Waziri Li Keqiang na kusisitiza, masaa machache baada ya China kushindwa kurudisha tozo kali kwa Marekani kama jibu la tozo madhubuti katika vita vya ushuru wa kuongezeka kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika tukio la Mkutano wa Uchumi wa Dunia katika mji wa bandari wa Tianjin kaskazini ya China Li hakutaja moja kwa moja mzozo wa biashara lakini alisema majadiliano ya kutaka Beijing kwa makusudi kudhoofisha sarafu yake ilikuwa “yasiyo na msingi.”
“Njia moja ya kushuka kwa Yuan huleta madhara zaidi kuliko faida kwa China,” alisema. “China kamwe haitatumia njia ya kutegemea kushuka kwa thamani ya Yuan ili kuchochea mauzo ya nje.”
China haitafanya hivyo ili kufukuzia “faida nyembamba” na “fedha ndogo ndogo”.
Li aliendelea kusema kwamba mfumo wa biashara ya maslahi ya wengi wa ulimwengu unapaswa kuzingatiwa, na kwamba vitendo vya kibiashara vya kujali nchi moja haitaweza kutatua matatizo yoyote kwa dunia ya leo.
Maneno yake yaliweza kuipa moyo Yuan ambayo imepoteza asilimia 9 ya thamani yake tangu katikati ya Aprili mwaka huu wakati wa vita vya biashara vinavyoendelea vya biashara kati yake na Marekani.
Beijing iliongeza tozo kwa bidhaa za thamani ya Dola bilioni 60 dhidi ya bidhaa za Marekani kwa orodha ya ushuru wa kuagiza kwa kulipiza kisasi kwa Rais wa Donald Trump iliyopangwa kwa bilioni 250 za bidhaa za Kichina.
Lakini Beijing iko radhi kupambana ili kukabiliana na ushuru wowote zaidi wa Marekani kwa msingi wa dola kwa dola, na kuinua wasiwasi inaweza kuchukua hatua nyingine zaidi kali kama anavyodai Rais Trumpa hadi isalimu amri kwani anadai kuwa ni hali ya hewa ya yajayo ambayo inaweza kuwa vita vya muda mrefu vya biashara.
Hata hivyo Uchina umesitisha ombi la mwaliko wa wiki iliyopita la Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin kushikilia mazungumzo mapya, ambayo China ilikubali wakati huo lakini sasa imesema hapana.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Geng Shuang alisema hakuwa na taarifa juu ya ujumbe wa biashara hiyo kuwezekana na kuhoji ukweli wa Marekani kuhusu kutaka mazungumzo mapya, akibainisha kuwa mzunguko wa mwisho ulifuatiwa mara moja na uanzishaji wa ushuru mpya. Hii ni sawa?
“Hii imekuwa aina ya utaratibu wa Marekani,” alisema Geng.
Marekani inataka kuishinikiza China kufanya mabadiliko makubwa kwa biashara yake, uhamisho wa teknolojia na sera za misaada ya viwanda vya juu.
Trump alikuwa amesema kuwa kulipiza kisasi na China ingeweza kusababisha ushuru wa bidhaa nyingine za Dola bilioni 267 za Kichina, juu ya majukumu ya dola bilioni 250 katika uagizaji ambao tayari umewekwa au kutishiwa.
China, ambayo ilinunua bidhaa dola 130 bilioni tu katika bidhaa za Marekani mwaka jana, imetoa au kutishia ushuru kwa dola bilioni 110 katika bidhaa za huko Marekani. Mashabiki hawakukosekana kwenye sakata hilo na kushabikia zaidi Marekani katika vita mfano wa Daudi na Goliath wa Biblia.
“China imeishiwa risasi kwani Mapambano yamefanyika na kwisha sasa ni swali la jinsi China inavyoweza kujisitiri aibu na kusema ‘hakika tutabadilika, itafungua upatikanaji kwa upana kwa kufungua masoko ya biashara sio tu kwa Marekani bali kwa Ulaya (EU) na Japan’, “alisema Christopher Peel, afisa wa uwekezaji mkuu katika Mali Tavistock huko London. Anasema
“Uchumi wao unaongozwa na kuuza nje ya nchi, hawawezi kumudu kuacha udhibiti,” aliiambia Reuters.
Athari za Bifu ya uchumi
Tozo za Ushuru mpya wa Marekani umeanza Septemba 24 kwa asilimia 10 na itaongezeka kwa asilimia hadi 25 mwishoni mwaka 2018, na Benki ya Amerika Merrill Lynch inatabiri kiwango cha asilimia 0.5 cha kushuka kwa ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka 2019 hadi asilimia 6.1.
Watafiti Oxford Economics walisema katika taarifa kwamba ukuaji wa kiuchumi wa China mwaka 2019 inaweza kuanguka chini ya asilimia 6, na kusema matarajio ya kuondokana na muda mrefu katika mvutano yalikuwa ya chini sana.
Lakini, imeongezea kuwa “uwezekano wa kuongezeka kwa uongezekaji utakuwepo kwa muda mrefu kama athari za kiuchumi zinazoongezeka kwa Marekani zitafanya timu ya Trump kupambana na China inajua kuwa itakuwa vigumu kuunganisha zaidi katika uchumi wa dunia bila makubaliano fulani kuhusu mfano wake wa kiuchumi hadi ueleweke!”
Wawekezaji walisisitizwa kuwa uongezekaji wa hivi karibuni ulikuwa mbaya zaidi kuliko washiriki wengine wa soko walivyotarajia, pamoja na hisa za Asia.
China bado haiogopi na inatamba kuwa “hatua kali” zilizochukuliwa na Marekani, gazeti la People’s Daily lilisema katika gazeti la ukurasa wa mbele katika toleo lake la nje ya nchi kuwa mapambano yataendelea mpaka kieleweke.”A luta continua. Mambo hayo.
Biashara na nchi nyingine
Kwa maana ya mfano na kufananisha ni Uhusiano wa kibiashara wa Marekani na Kanada ambao kwa miaka ya karibuni ulikuwa na ukubwa wa pili duniani baada ya China na Marekani. Mnamo mwaka juzi (2016), biashara na bidhaa za biashara kati ya nchi hizo mbili zilifikia dola bilioni 627.8.
Uuzaji wa Marekani ulikuwa dola bilioni 320.1 wakati uagizaji ulikuwa dola bilioni 307.6 na hivi basi kufanya Marekani kuwa na ziada ya dola bilioni 12.5 kwa Kanada.
Kanada imekuwa na historia ya upungufu wa biashara na Marekani kila mwaka tangu mwaka 1985 katika biashara halisi ya bidhaa, isipokuwa huduma. Uhusiano wa biashara kati ya nchi hizo mbili huvuka viwanda vyote na ni muhimu kwa mafanikio ya mataifa yote kama kila nchi ni mojawapo ya washirika wa biashara kubwa zaidi.
Yaani Biashara kati ya Daraja la Embassy (Balozi Bridge,) kati ya Windsor, Ontario na Detroit, Michigan, peke yake ni sawa na biashara zote kati ya Marekani na Japan.
Ukiendeleza mbali zaidi na Mexico kwenye Jumuia ya NAFTA utaona tatizo na athari za maamuzi holela ya Rais Trump. Lakini Rais Trump amemtishia Waziti Mkuu Justine Trudeau wa Kanada kuwa NAFTA itazamwe upya na anataka kuongeza vikwazo na kama sio kuufuta mkataba huo.
Kwa nini China?
Uhusiano wa kimataifa kati ya China na Marekani ni mkubwa lakini bado ni mgumu kwenye masuala mengi. Nchi zote mbili zina ushirikiano mkubwa sana wa kiuchumi, na kiasi kikubwa cha biashara kati ya nchi hizo mbili kinahitaji uhusiano mzuri wa kisiasa, lakini masuala muhimu yaliyopo yanahitaji juhudi ya kuyamaliza. Ni ushirikiano wa kiuchumi, ushindani wa dola katika Pasifiki, na mashaka ya pamoja juu ya nia za wengine.
Kwa hiyo, kila taifa limechukua mtazamo wa kutosha juu ya mwingine kama mpinzani anayeweza kuwa wakati huo huo kuwa mpenzi mkubwa wa kiuchumi.
Imeelezewa na viongozi wa dunia na wasomi kama uhusiano muhimu zaidi wa nchi na nchi kwa karne ya 21.
Mnamo mwaka wa 2018, Marekani ina uchumi mkubwa duniani na China ina ukubwa wa pili, kwa maelezo ya IMF na Benki ya Dunia ingawa China ina GDP kubwa kwa kipimo cha PPP. Marekani ina utajiri mkubwa wa kitaifa (national wealth) kutokana na maendeleo yake katika sekta za jamii na maendeleo ya huduma.
Uhusiano kati ya nchi mbili hizi kwa ujumla umekuwa imara na baadhi ya vipindi vya migogoro ya wazi, hasa wakati wa vita vya Korea miaka ya 1950 na vita vya Vietnam (1970), ambapo China ilimsaidia Vietnam na kumshinda Marekani.
Kwa sasa, China na Marekani wana masilahi ya kisiasa, ya kiuchumi na ya usalama, lakini si tu kwa kuenea kwa silaha za nyuklia, ingawa kuna matatizo yasiyotatuliwa yanayohusiana na jukumu la demokrasia katika Serikali nchini China na haki za binadamu katika nchi zote mbili. China ni deni kubwa zaidi la kigeni la Marekani.
Nchi hizo mbili zinabakia katika mgogoro juu ya masuala ya taifa katika Bahari ya Kusini ya China na visiwa vilivyojengwa na China kwenye mkondo wa biashara wa Bahari ya China ikidaiwa ni kupora eneo.
Maoni ya umma ya nchi nyingine (public opinion) huelekea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 40 hadi 50. Kufikia mwaka wa 2015, maoni ya umma ya China kuhusu Marekani ni asilimia 44, wakati maoni ya umma ya Marekani ya China ni kidogo chini ya asilimia 38.
Maoni yaliyo bora sana ya Marekani yalikuwa ya asilimia 58 katika mwaka 2010 na ya chini kabisa kwa 38 kwa mwaka 2007.
Kinyume chake, maoni yaliyo bora zaidi ya China yalikuwa ya asilimia 52 kwa mwaka 2006 na chini ya asilimia 35 ya mwaka 2014.
Uhusiano na China ulianza chini ya George Washington aliyeongoza Marekani katika mk.ataba wa mwaka 1845 wa Wangxia.
Marekani ulihusishwa na Jamhuri ya China (Taiwan) wakati wa vita vya Pasifiki, lakini ilivunja mahusiano na China kwa miaka 25 wakati Serikali ya kikomunisti ilipochukua mamlaka mwaka 1949 mpaka ziara ya Rais Richard Nixon ya mwaka 1972 nchini China.
Tangu Nixon, rais wote wa Marekani kwa mfululizo wamekwenda China.
Mahusiano na Uchina yameshindwa chini ya mkakati wa kutoingilia upande (pivot) wa Barack Obama wa Asia, msaada wa Marekani kwa Japan katika mgogoro wa visiwa vya Senkaku, pamoja na vitisho vya Donald Trump kugawa nchi kama ‘mshahabishaji fedha’ (currency manipulator ) kama sehemu ya vita vya kibiashara vinavyoendelea .
Wakati huo huo mjini Paris, Rais wa Ufaransa Emanuel Macron aushutumu mtazamo wa Trump wa ‘mwenye nguvu mpishe’ unaofanywa na nchi kubwa duniani.
Rais Macron wa Ufaransa amewaomba viongozi wa dunia kupinga kile alichokitaja sheria ya ‘mwenye nguvu kuliko wote mpishe’; alikuwa akikosoa vikali mtizamo wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kushughulikia kivyake changamoto zinazoikumba dunia bila kumtaja yeye kwa jina, lakini hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliainisha misimamo ambayo ni tofauti kabisa na mtazamo alionao rais huyo wa Marekani.
Macron alisema: “Baadhi ya viongozi wameamua kufuata sheria ya mwenye nguvu mpishe. Lakini hilo haliwezi kumlinda yeyote, badala yake naunga mkono ushirikiano na mashauriano yanayoshirikisha pande zote kama msingi wa Umoja wa Mataifa na juhudi za kufikiwa amani duniani.”
Kiongozi huyo wa Ufaransa pia amesema kuongezeka kwa ukosefu wa usawa wa kiuchumi ni moja ya vichocheo vya mizozo, huku takriban watu milioni 783 duniani wakiishi katika umasikini na watoto milioni 250 wakikosa elimu.
Lakini wachunguzi wa mambo ya dunia wanasema dunia inakosea kumweka Trump pekee na si serikali yake, kwani hakuna kitu kama hicho kwani kile anachofanya Trump kinyume na ulimwengu wote ni mahitaji sahihi ya Wamarekani ndio maana wananchi na chama pingamizi cha Democratic hakijatoa neno wala kudadisi vitendo hivyo vya kizuvendi vya Trump. Ni mfano tosha wa mtazamo tofauti wa Marekani na dunia nyingine kwani yenyewe ni Dola ya Marekani.